Jumanne. 22 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

Kumbukumbu ya Yohane Chrisostom, Askofu na Daktari wa Kanisa (Ijumaa, Septemba 13, 2024)  

Somo la 1

1Kor 9:16–19, 22–27

Ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri Injili! Maana nikiitenda kazi hii kwa hiari yangu nina thawabu; ila ikiwa si kwa hiari yangu, nimeaminiwa uwakili. Basi thawabu yangu ni nini? Ni hii, ya kuwa nihubiripo, nitaitoa Injili bila gharama, bila kutumia kwa utimilifu uwezo wangu nilio nao katika Injili. Maana, ingawa nimekuwa huru kwa watu wote, nalijifanya mtumwa wa wote, ili nipate watu wengi zaidi. Kwa unyonge nalikuwa mnyonge, ili niwapate wanyonge. Nimekuwa hali zoTe kwa watu wote, ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu. Nami nafanya mambo yote kwa ajili ya Injili ili kuishiriki pamoja na wengine. Je! Hamjui, ya kuwa wale washindanao kwa kupiga mbio, hupiga mbio wote lakini apokeaye tuzo ni mmoja? Pigeni mbio namna hiyo, ili mpate. Na kila ashindanaye katika michezo hujizuia katika yote; basi hao hufanya hivyo kusudi wapokee taji iharibikayo; bali sisi tupokee taji isiyoharibika. Hata mimi napiga mbio vivyo hivyo, si kama asitaye; napiga ngumi vivyo hivyo, si kama apigaye hewa; bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; Isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.

Wimbo wa Katikati

Zab 84:2–5, 7, 11

Nafsi yangu imeziona shauku nyua za Bwana,
Naam, na kuzikondea.
Moyo wangu na mwili wangu
Ninamlilia Mungu aliye hai.
(K) Maskani zao zapendeza kama nini, Ee Bwana wa majeshi.

Shomoro naye ameona nyumba,
Na mbayuwayu amejipatia kioto,
Alipoweka makinda yanke,
Kwenye madhabahu zako, Ee Bwana wa majeshi,
Mfalme wangu na Mungu wangu.
(K) Maskani zao zapendeza kama nini, Ee Bwana wa majeshi.

Heri wakaao nyumbani mwako,
Wanakuhimidi daima.
Heri ambaye nguvu zake zatoka kwako,
Na njia ziendazo Sayuni zimo moyoni mwake.
Huendelea toka nguvu hata nguvu,
Huonekana Sayuni kila mmoja mbele za Mungu.
(K) Maskani zao zapendeza kama nini, Ee Bwana wa majeshi.

Kwa kuwa Bwana, Mungu, ni jua na ngao,
Bwana atatoa neema na utukufu.
Hatawanyima kitu chema
Hao waendao kwa ukamilifu.
(K) Maskani zao zapendeza kama nini, Ee Bwana wa majeshi.

Shangilio

Mt 11:25

Aleluya, aleluya,
Nakushukuru Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga.
Aleluya.

Injili

Lk 6:39–42

Yesu aliwaambia wanafunzi wake mithali, Je! Aliye kipofu aweza kuongoza kipofu? Hawatatumbukia shimoni wote wawili? Mwanafunzi hawi mkuu kuliko mwalimu wake, lakini kila mtu ambaye amehitimu hulingana na mwalimu wake. Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenye huiangalii? Au, utawezaje kumwambia ndugu yako, Ndugu yangu, niache nikitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako, nawe huiangalii boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafikiri wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu yako.

Maoni


Ingia utoe maoni