Jumatano. 30 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

Ijumaa ya 1 ya Majilio (Ijumaa, Desemba 02, 2016)  

Somo la 1

Isa 29:17-24

Je! Si muda mdogo uliobaki, na Lebanoni itageuzwa kuwa shamba lizaalo sana, na lile shamba lizaalo sana litahesabiwa kuwa msitu? Na katika siku hiyo viziwi watasikia maneno ya hicho chuo, na macho ya vipofu yataona katika upofu na katika giza. Wanyenyekevu nao wataongeza furaha yao katika Bwana, na maskini katika wanadamu watafurahi katika Mtakatifu wa Israeli. Kwa maana mwenye kutisha ameangamizwa, naye mwenye dharau amekoma, nao wote watazamiao uovu wamekatiliwa mbali; hao wamfanyao mtu kuwa amekosa katika neno, na kumtegea mtego yeye aonyaye langoni, na kumgeuza mwenye haki kwa kitu kisichofaa. Basi, Bwana aliyemkomboa Ibrahimu asema hivi, katika habari za nyumba ya Yakobo; Yakobo hatatahayarika sasa, wala uso wake hautabadilika rangi yake. Bali atakapowaona watoto wake, walio kazi ya mikono yangu, katikati yake, wao watalitakasa jina langu; naam, watamtakasa Mtakatifu wa Yakobo, nao watamcha Mungu wa Israeli. Hao nao wakosao rohoni mwao watapata kufahamu, na hao wanung'unikao watajifunza elimu.

Wimbo wa Katikati

Zab 27:1, 4, 13-14

Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani?
(K) Bwana ni nuru na wokovu wangu.

Neno Moja nimelitaka kwa Bwana, Nalo ndilo nitakalolitafuta,
Nikae nyumbani mwa Bwana Siku zote za maisha yangu,
Niutazame uzuri wa Bwana, Na kutafakari hekaluni mwake.
(K) Bwana ni nuru na wokovu wangu.

Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana Katika nchi ya walio hai.
Umngoje Bwana, uwe hodari, Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana.
(K) Bwana ni nuru na wokovu wangu.

Shangilio

Shangilio

Aleluya, aleluya,
Tazama Bwana wetu atakuja na nguvu, Na atayaangaza macho ya watumishi wake.
Aleluya.

Injili

Mt 9:27-31

Siku ile: Yesu alipokuwa akipita kutoka huko, vipofu wawili wakamfuata wakipaza sauti, wakisema, Uturehemu, Mwana wa Daudi. Naye alipofika nyumbani, wale vipofu walimwendea; Yesu akawaambia, Mnaamini kwamba naweza kufanya hili? Wakamwambia, Naam, Bwana. Ndipo alipowagusa macho, akasema, Kwa kadiri ya imani yenu mpate. Macho yao yakafumbuka. Naye Yesu akawaagiza kwa nguvu, akisema, Angalieni hata mtu mmoja asijue. Lakini wakatoka, wakaeneza habari zake katika nchi ile yote.

Maoni


Ingia utoe maoni