Jumatano. 30 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

Jumamosi ya 1 ya Majilio (Jumamosi, Desemba 03, 2016)  

Somo la 1

Isa 30:19-21, 23-26

Bwana Mungu Mtakatifu wa Israeli asema: Kwa maana watu watakaa katika Sayuni huko Yerusalemu; wewe hutalia tena; hakika yake atakuonea rehema nyingi kwa sauti ya kilio chako; asikiapo ndipo atakapokujibu. Na ingawa Bwana atawapeni chakula cha shida na maji ya msiba, lakini waalimu wako hawatafichwa tena, ila macho yako yatawaona waalimu wako; na masikio yako yatasikia neno nyuma yako, likisema, Njia ni hii, ifuateni; mgeukapo kwenda mkono wa kulia, na mgeukapo kwenda mkono wa kushoto. Naye atatoa mvua juu ya mbegu zako, upate kuipanda nchi hii; na mkate wa mazao ya nchi, nayo itasitawi na kuzaa tele; katika siku hiyo ng'ombe zako watakula katika malisho mapana. Ng'ombe pia na wana-punda wailimao nchi watakula chakula kilichokolea, kilichopepetwa kwa ungo na kwa pepeo. Na juu ya kila mlima mrefu, na juu ya kila kilima kilichoinuka, itakuwapo mito na vijito vya maji, katika siku ya machinjo makuu itakapoanguka minara. Na tena nuru ya mwezi itakuwa kama nuru ya jua, na nuru ya jua itaongezeka mara saba, kama nuru ya siku saba, katika siku ile Bwana atakapofunga mapigo ya watu wake, na kuliponya pigo la jeraha yao.

Wimbo wa Katikati

Zab 147:1-6

Aleluya. Msifuni Bwana; Maana ni vema kumwimbia Mungu wetu,
Maana kwapendeza, kusifu ni kuzuri.
Bwana ndiye aijengaye Yerusalemu,
Huwakusanya waliotawanyika wa Israeli.
(K) Heri wote wamngojeao Bwana.

Huwaponya waliopondeka moyo,
Na kuziganga jeraha zao.
Huihesabu idadi ya nyota,
Huzipa zote majina.
(K) Heri wote wamngojeao Bwana.

Bwana wetu ni mkuu na mwingi wa nguvu,
Akili zake hazina mpaka.
Bwana huwategemeza wenye upole,
Huwaangusha chini wenye jeuri.
(K) Heri wote wamngojeao Bwana.

Shangilio

Isa. 33:22

Aleluya, aleluya.
Bwana ndiye mwamuzi wetu; Bwana ndiye mfanya sheria wetu; Bwana ndiye mfalme wetu; Ndiye atakayetuokoa.
Aleluya.

Injili

Mt 9:35- 10:1, 6-8

Siku ile: Yesu alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri habari njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji. Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake.Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia. Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.

Maoni


Ingia utoe maoni