Masomo ya Misa
Alhamisi ya 12 ya Mwaka (Alhamisi, Juni 27, 2024)
2 Fal 24:8-17
Yekonia alikuwa na umri wa miaka kumi na minane alipoanza kutawala; akatawala miezi mitatu katika Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Nehushta binti Elnathani wa Yerusalemu. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, mfano wa yote aliyoyafanya baba yake. Wakati ule watumishi wa Nebukadreza mfalme wa Babeli wakakwea kwenda Yerusalemu, na mji ukahusuriwa. Na Nebukadreza, mfalme wa Babeli, akaufikilia huo mji, hapo watumishi wake walipokuwa wakiuhusuru.Na Yekonia, mfalme wa Yuda, akatoka akamwendea mfalme wa Babeli, yeye na mama yake, na watumishi wake, na wakuu wa watu wake, na maakida wake; mfalme wa Babeli akamchukua mateka katika mwaka wa nane wa kutawala kwake. Akatoa huko hazina zote za nyumba ya Bwana, na hazina za nyumba ya mfalme, akavikata-kata vyombo vyote vya dhahabu ambavyo Sulemani, mfalme wa Israeli, alivifanya katika hekalu la Bwana, kama Bwana alivyosema. Akawachukua mateka watu wa Yerusalemu wote pia, na wakuu wote, na mashujaa wote, watu elfu kumi; na mafundi wote, na wafua chuma wote; hapana mtu aliyebaki, ila waliokuwa wanyonge wa watu wa nchi. Akamchukua Yekonia mpaka Babeli; na mama yake mfalme, na wake zake mfalme, na maakida wake, na wakuu wa nchi, aliwachukua mateka toka Yerusalemu mpaka Babeli. Na mashujaa wote, watu elfu saba, na mafundi na wafua chuma elfu moja, wote pia wenye nguvu, tayari kwa vita, hao wote mfalme wa Babeli aliwachukua mateka mpaka Babeli. Mfalme wa Babeli akamtawaza Matania, ndugu ya baba yake, awe mfalme badala yake, akalibadili jina lake, akamwita Sedekia.
Zab 79:1-5, 8-9
Ee Mungu, mataifa wameingia katika urithi wako,
Wamelinajisi hekalu lako takatifu.
Wamefanya Yerusalemu chungu chungu.
Wameziacha maiti za watumishi wako Ziwe chakula cha ndege wa angani.
Na miili ya watauwa wako Iwe chakula cha wanyama wa nchi.
(K)Utuokoe Ee Bwana, kwa ajili yaa jina lako.
Wamemwaga damu yao kama maji Pande zote za Yerusalemu, Wala hapakuwa na mzishi.
Tumekuwa lawama kwa jirani zetu, Mzaha na dhihaka kwao wanaotuzunguka.
Ee Bwana, hata lini? Utaona hasira milele? Wivu wako utawaka kama moto?
(K)Utuokoe Ee Bwana, kwa ajili yaa jina lako.
Usikumbuke juu yetu maovu ya baba zetu,
Rehema zako zije kutulaki hima,
Kwa maana tumedhilika sana.
(K)Utuokoe Ee Bwana, kwa ajili yaa jina lako.
Ee Mungu wa wokovu wetu, utusaidie, Kwa ajili ya utukufu wa jina lako.
Utuokoe, utughofiri dhambi zetu, Kwa ajili ya jina lako.
(K)Utuokoe Ee Bwana, kwa ajili yaa jina lako.
Yn 14:23
Aleluya, aleluya
Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake.
Aleluya
Mt 7:21-29
Yesu aliwaambia wanafunzi wake; Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu. Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa. Ikawa, Yesu alipoyamaliza maneno hayo, makutano walishangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi wao.
Maoni
Ingia utoe maoni