Alhamisi, Juni 27, 2024
Alhamisi, Juni, 27, 2024,
Tafakari ya kila siku
Juma la 12 la Mwaka wa Kanisa
2 Fal 24: 8-17;
Zab 78: 1-5, 8-9;
Mt 7: 21-29
NAWEZAJE KUINGIA KATIKA UFALME WA MUNGU?
Ni nani ataingia katika ufalme wa Mungu au mtu gani awezaye kuingia katika ufalme wa Mungu? Ni swali ambalo tunalisikia mara nyingi kutoka kwa watu. Kijana mmoja tajiri anakuja kwa Yesu na anauliza swali hilo hilo (Mk 10: 17-31). Leo katika Injili Yesu anatoa jibu la swali hili, FANYA MAPENZI YA MUNGU (Mt 7: 21). Mapenzi ya Mungu yanafunuliwa kwetu kwa njia mbali mbali. Anayesoma neno la Mungu nakulitafakari atatambua Mungu anataka nini kwake. Yule ambaye anasikiliza pia dhimiri yake na kusikiliza wengine pia atayatambua mapenzi ya Mungu. Yesu aliwafundisha wafuasi wake na pia anatufundisha sisi jinsi yakufanya mapenzi ya Mungu. Wakati aliposema “Mpende Mungu kwa Moyo wako wote na akili yako yote na mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe” (Lk 10: 27), alikuwa anafunua mapenzi ya Mungu kwa wafuasi wake. Maisha ya mtu yakijazwa mapendo kwa Mungu na jirani huyu anayafanya mapenzi ya Mungu. Kwahiyo kwa njia hii ataingia katika ufalme wa Mungu
Maisha ya mtu mwenye hekima, anayelisikia neno la Mungu na kufanya mapenzi ya Mungu, ni kama nyumba iliyojengwa kwenye mwamba mgumu. Hata kama kuna mateso, maumivu, uchungu na matatizo atakuwa na nguvu ya kusimama imara na yote yatapita. Lakini anayesikia neno la Mungu na halitendi atakuwa kama mtu aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga, Yesu alisema. Atatetereka atakapo patwa na matatizo madogo au changamoto za maisha. Leo tunapaswa kuuchukua mfano huu wa Yesu. Alisema “chakula changu nikutenda mapenzi ya Baba yangu” (Yn 4: 34). Akimaanisha kuyafanya mapenzi ya Mungu yaliyo kila kitu katika maisha yake. Tuombe neema yakutenda mapenzi ya Mungu katika maisha yetu.
Sala:
Bwana ni ngome yangu, mwamba wangu, na mwokozi wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia, kinga yangu na pembe ya wokovu wangu na nguvu zangu. (Zab 18: 2).
Amina
Maoni
Ingia utoe maoni