Masomo ya Misa
Dominika ya 11 ya Mwaka (Jumapili, Juni 16, 2024)
Eze 17:22-24
Bwana Mungu asema hivi; Mimi nami nitakitwaa kilele kirefu cha mwerezi, na kukipandikiza mahali; na katika vitawi vyake vilivyo juu nitatwaa kitawi kimoja kilicho chororo, nami nitakipanda juu ya mlima mrefu ulioinuka sana; juu ya mlima wa mahali palipoinuka pa Israeli nitakipanda; nacho kitatoa matawi, na kuzaa matunda, nao utakuwa mwerezi mzuri; na chini yake watakaa ndege wa kila namna ya mbawa; katika uvuli wa matawi yake watakaa. Na miti yote ya mashamba itajua ya kuwa mimi, Bwana, nimeushusha chini mti mrefu, na kuuinua mti mfupi, na kuukausha mti mbichi, na kuusitawisha mti mkavu; mimi, Bwana, nimenena, nami nimelitenda jambo hili.
Zab 92:1 -2 ,12 -15
Ni neno jema kumshukuru Bwana,
Na kuliimba jina lako, Ee Uliye juu.
Kuzitangaza rehema zako asubuhi,
Na uaminifu wako wakati wa usiku.
(K) Ni neno jema kumshukuru Bwana.
Mwenye haki atasitawi kama mtende,
Atakua kama mwerezi wa Lebanoni.
Waliopandwa katika nyumba ya Bwana
Watasitawi katika nyua za Mungu wetu.
(K) Ni neno jema kumshukuru Bwana.
Watazaa matunda hadi wakati wa uzee,
Watajaa utomvu, watakuwa na ubichi.
Watangaze ya kuwa Bwana ni mwenye adili.
Mwamba wangu, ndani yake hamna udhalimu.
(K) Ni neno jema kumshukuru Bwana.
2Kor 5:6-10
Sikuzote tuna moyo mkuu; tena twajua ya kuwa. wakati tuwapo hapa katika mwili, tunakaa mbali na Bwana. (Maana twaenenda kwa imani, si kwa kuona.) Lakini tuna moyo mkuu; nasi tunaona ni afadhali kutokuwamo katika mwili na kukaa pamoja na Bwana. Kwa hiyo, tena, ikiwa tupo hapa, au ikiwa hatupo hapa, twajitahidi kumpendeza yeye. Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya.
Yn 6:63, 68
Aleluya, aleluya,
Bwana, maneno yako ni roho tena ni uzima.
Aleluya.
Mk 4:26-34
Yesu alisema, Ufalme wa Mungu, mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi; akawa akilala na kuondoka, usiku na mchana, nayo mbegu ikamea na kukua, asivyojua yeye. Maana nchi huzaa yenyewe; kwanza jani, tena suke, kisha ngano pevu katika suke. Hata matunda yakiiva, mara aupeleka mundu, kwa kuwa mavuno yamefika. Akasema, Tuulinganishe na nini ufalme wa Mungu? au tuutie katika mfano gani? Ni kama punje ya haradali, ambayo ipandwapo katika nchi, ingawa ni ndogo kuliko mbegu zote zilizo katika nchi, lakini ikiisha kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi makubwa; hata ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake. Kwa mifano mingi ya namna hii alikuwa akisema nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulisikia; wala pasipo mfano hakusema nao; lakini akawaeleza wanafunzi wake mwenyewe mambo vote kwa faragha.
Maoni
Ingia utoe maoni