Jumanne. 16 Julai. 2024

Tafakari

Jumapili, Juni 16, 2024

Jumapili, Juni 16, 2024
Dominika ya 11 ya Mwaka

Eze 17:22-24;
Zab 92: 1-2,12-15 (K. 1);
2 Kor 5:6-10;
Mk 4:26 -34.

KUIENDELEZA MBEGU YA IMANI NDANI YAKO!

Katika somo la Kwanza nabii Ezekieli anatabiri kwamba Johakim, Mwana wa mwisho katika shina la Daudi, atashindwa na kukamatwa na kupelekwa utumwani Babeli. Hili janga la kitaifa lilitikisa Imani ya Wayahudi wengi, kwasababu Mungu alikuwa ameahidi kwamba utawala wa Daudi utatawala milele. Sasa Mungu amesahau ahadi yake kwa wateule wake? Lakini pia katika unabii huu kuna ahadi kwamba katika shina hili la Daudi lililo haribiwa Mungu atachipusha mbegu ndogo ambaye itakuwa na kuwa mti mkubwa na ndege wa kila aina watajenga kiota na kukaa ndani yake.

Yesu katika somo la Injili kutoka Injili ya Marko anaelezea ukuwaji wa Ufalme wa Mungu kwa kutumia mfano. Umegawanyika katika sehemu tatu katika hali tofauti, ukilinganishwa na hali tatu za mkulima, kusia mbegu, kuota na kuvuna. Katika hali ya kwanza na ya tatu ndipo kazi ya mkulima inapo elezewa, “anatawanya mbegu katika ardhi” na “kuotesha” hakuna la ziada. Huyu mwandishi lengo lake kubwa alitaka kulenga katika ukuwaji wa hii mbegu.

Yesu yupo katika hali ya kuelezea nguvu ya mbegu ilivyo ambayo haisaidiwi bali inaota kwa kupasua ardhi na kuota. Mwinjili hakutumia neno la kawaida la kusia, lakini anaeleza kuhusu mtu ambaye anatapanya mbegu, akionesha kwamba furaha ya mkulima alivyokuwa akifanya kirahisi kwa mkono wake akitawanya mbegu kila mahali. Neno la Mungu au Injili ya Yesu inapaswa kutapanywa katika hali hii, kuhubiriwa katika hali hii, sio katika sehemu tuu au watu tuu maalumu bali kwa watu wote, kila mahali kwa maana kwamba ulimwenguni kote. Mungu mwenyewe ndiye atasaidia iweze kuota.

Muda ambao mtu anapumzika na kuacha kufanya kazi ni baada ya kuotesha. Usiku na mchana mkulima anaenda kutazama na hata kulala bila kuingilia ukuwaji wake. Hana lakufanya isipokuwa kusubiri. Tena kwa ukimya na katika hali ya uvumilivu na hapo muujiza huanza: mbegu inakuwa na kuchomoza kutoka ardhini. Maelezo ya ukuaji yanaeleweka kwanza shina linatokea na hali ya kijani hujitokeza baadae huzaa mavuno yake. Ni muda ambao unapaswa kusibiri huwezi kutumia nguvu. Ni wakati wa subira na uvumilivu. Ndivyo neno la Mungu linavyokuwa ndani mwetu.

Siku mmoja katika Parokia moja Padre aliulizwa na mwanaparokia wake, kijana wa kiume. “nilijaribu kusoma Biblia kama wewe lakini sielewi, na ninachokielewa ninakisahau mara moja ninapofunga tu kitabu. Sasa Napata nini ninapo soma Biblia?

Wakati huo Padre alikuwa anapika, kwa ukimya aligeuka kutoka kuweka mkaa katika jiko na alisema, “Beba kikapu hiki cha mkaa peleka mtoni na niletee maji.” Yule kijana alifanya kadiri alivyoambiwa, maji yote yalivuja kabla hata hajafikisha nyumbani. Padre alicheka na alisema, “wakati ujao utatakiwa utembee kwa haraka zaidi,” na alimrudisha tena mtoni akiwa na kikapu ili ajaribu tena. Wakati huu yule kijana alikimbia sana, lakini tena kikapu kilikuwa tupu kabla ya kufika nyumbani. Akiwa anahema alimwambia Padre kwamba “haiwezekana kubeba maji katika kikapu,” na badala yake alikwenda kuchukua ndoo. Mzee alisema, “sihitaji ndoo ya maji; ninataka ubebe maji na kikapu hiki hiki.” Wewe unaweza kufanya hivyo. Jaribu tena ila kimbia kwa mwendo mkali zaidi. Padre akaenda nje mlangoni kumwangalia yule kijana wa kiume akijaribu tena. Wakati huu, kijana alijua kuwa haikuwezekana, lakini alitaka kumuonyesha Padre kuwa hata kama angekimbia sana kiasi alichoweza, maji yangevuja yote kabla hata ya kufika mbali. Kijana alijaza maji vizuri na alikimbia vizuri sana, lakini alipofika kwa Padre, tena kikapu kilikuwa kitupu.

Akiwa anahema sana alisema, “Angalia, hakuna maana!” Padre alisema, “Angalia angalia ndani ya kapu na kapu lenyewe.” Kijana aliangalia na kwa mara ya kwanza aligundua kuwa kikapu kilionekana tofauti. Badala ya kuwa kikapu cha mkaa kikavu cha zamani, kilikuwa kimetakata. “Mwanangu, hivyo ndivyo vinavyotokea pale unaposoma Biblia. huenda usielewe au kukumbuka kila kitu, lakini unapoisoma, itakubadilisha wewe toka ndani mpaka nje taratibu taratibu kama vile mbegu unavyokuwa. Hiyo ndiyo kazi ya Imani ya Mungu ndani mwetu. Kutubadilisha sisi kutoka ndani mpaka nje na taratibu kutubadilisha sisi tuweze kuwa na sura ya Mwanae.

Hivyo pia, Injili ya leo inaongelea juu ya Mifano ya mbegu na mpanzi, na mbegu ya haradali. Mungu amepanda mbegu ndani ya mioyo yetu, inaweza kukuwa katika mti mkubwa na kuzaa matunda mia zaidi. Lakini swali tunalotakiwa kujiuliza wenyewe, je, Mimi ni kama yule kijana wa kiume nimefanya juhudi za kwenda mtoni, hata kama nilijua kuwa haikuwa na maana kuleta maji ndani ya kikapu, au nimekata tamaa? Basi wiki hii tuwe wakimya! Ukimya katika kusikiliza Neno la Mungu kadiri linavyosafisha na kututakasa tubadilishwe katika sura ya Yesu.

Sala:
Bwana, nisikilize ninapoongea nawe, Neno lako kila siku linigeuze moyo na akili yangu viwe kwa Yesu.
Amina

Maoni


Ingia utoe maoni