Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumatano ya 33 ya Mwaka (Jumatano, Novemba 16, 2016)  

Somo la 1

Ufu 4:1-11

Mimi Yohane, niliona mlango ukafunguka mbinguni, na sauti ile ya kwanza niliyoisikia kama sauti ya baragumu ikinena nami, ikisema, Panda hata huku, nami nitakuonyesha mambo ambayo hayana budi kuwako baada ya hayo. Na mara nalikuwa katika Roho; na tazama, kiti cha enzi kimewekwa mbinguni na mmoja ameketi juu ya kile kiti; na yeye aliyeketi alionekana mithili ya jiwe la yaspi na akiki, na upinde wa mvua ulikizunguka kile kiti cha enzi, ukionekana mithili ya zumaridi. Na viti ishirini na vinne vilikizunguka kile kiti cha enzi, na juu ya vile viti naliona wazee ishirini na wanne, wameketi, wamevikwa mavazi meupe; na juu ya vichwa vyao walikuwa na taji za dhahabu. Na katika kile kiti cha enzi kunatoka umeme na sauti na ngurumo. Na taa saba za moto zilikiwaka mbele ya kile kiti cha enzi, ndizo Roho saba za Mungu. Na mbele ya kile kiti cha enzi kulikuwa na mfano wa bahari ya kioo, kama bilauri; na katikati ya kile kiti cha enzi, na pande zote za kile kiti, walikuwako wenye uhai wanne, wamejaa macho mbele na nyuma. Na huyo mwenye uhai wa kwanza alikuwa mfano wa simba; na mwenye uhai wa pili alikuwa mfano wa ndama; na mwenye uhai wa tatu alikuwa na uso kama uso wa mwanadamu; na mwenye uhai wa nne alikuwa mfano wa tai arukaye. Na hawa wenye uhai wanne, kila mmoja alikuwa na mabawa sita; na pande zote na ndani wamejaa macho, wala hawapumziki mchana wala usiku, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu Mwenyezi, aliyekuwako na aliyeko na atakayekuja. Na hao wenye uhai wanapompa yeye aketiye juu ya kiti cha enzi utukufu, na heshima, na shukrani, yeye aliye hai hata milele na milele, ndipo hao wazee ishirini na wanne huanguka mbele zake yeye aketiye juu ya kile kiti cha enzi, nao humsujudia yeye aliye hai hata milele na milele, nao huzitupa taji zao mbele ya kile kiti cha enzi, wakisema, Umestahili wewe, Bwana wetu na Mungu wetu, kuupokea utukufu na heshima na uweza; kwa kuwa wewe ndiwe uliyeviumba vitu vyote, na kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako, navyo vikaumbwa.

Wimbo wa Katikati

Zab 150

Msifuni Mungu katika patakatifu pake;
Msifuni katika anga la uweza wake.
Msifuni kwa matendo yake makuu;
Msifuni kwa kadiri ya wingi wa ukuu wake.
(K) Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu wa Mwenyezi

Msifuni kwa mvumo wa baragumu;
Msifuni kwa kinanda na kinubi;
Msifuni kwa matari na kucheza;
Msifuni kwa zeze na filimbi;
(K) Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu wa Mwenyezi

Msifuni kwa matoazi yaliayo;
Msifuni kwa matoazi yavumayo sana.
Kila mwenye pumzi na amsifu Bwana. Aleluya.
(K) Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu wa Mwenyezi

Shangilio

Yn. 8:12

Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, asema Bwana, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.
Aleluya.

Injili

Lk 19:11-28

Makutano waliposikia hayo, aliongeza kusema mfano, kwa sababu alikuwa karibu na Yerusalemu, na wao walidhani ya kuwa ufalme wa Mungu utaonekana mara. Basi akasema, Mtu mmoja, kabaila, alisafiri kwenda nchi ya mbali, ili ajipatie ufalme na kurudi. Akaita watu kumi katika watumwa wake, akawapa mafungu kumi ya fedha, akawaambia, Fanyeni biashara hata nitakapokuja. Lakini watu wa mji wake walimchukia, wakatuma wajumbe kumfuata na kusema, Hatumtaki huyu atutawale. Ikawa aliporudi, ameupata ufalme wake, aliamuru waitwe wale watumwa aliowapa fedha, ili ajue faida aliyopata kila mtu kwa biashara yake. Akaja wa kwanza, akasema, Bwana, fungu lako limeleta faida ya mafungu kumi zaidi. Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi. Akaja wa pili, akasema, Bwana, fungu lako limeleta mafungu matano faida. Akamwambia huyu naye, Wewe uwe juu ya miji mitano. Akaja mwingine akasema, Bwana, hili ndilo fungu lako, ambalo nililiweka akiba katika leso. Kwa maana nilikuogopa kwa kuwa u mtu mgumu; waondoa usichoweka, wavuna usichopanda. Akamwambia, Nitakuhukumu kwa kinywa chako, mtumwa mwovu wewe. Ulinijua kuwa ni mtu mgumu, niondoaye nisichoweka, na kuvuna nisichopanda; basi, mbona hukuiweka fedha yangu kwa watoao riba, ili nijapo niipate pamoja na faida yake? Akawaambia waliosimama karibu, Mnyang'anyeni hilo fungu, mkampe yule mwenye mafungu kumi. Wakamwambia, Bwana, anayo mafungu kumi. Nawaambia, Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang'anywa hata alicho nacho. Tena, wale adui zangu, wasiotaka niwatawale, waleteni hapa mwachinje mbele yangu. Na alipokwisha kusema hayo, alitangulia mbele akipanda kwenda Yerusalemu.

Maoni


Ingia utoe maoni