Jumatano. 30 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

Jumanne ya 32 ya Mwaka (Jumanne, Novemba 08, 2016)  

Somo la 1

Tit 2: 1-8, 11-14

Lakini wewe nena mambo yapasayo mafundisho yenye uzima; ya kwamba wazee wawe wenye kiasi, wastahivu, wenye busara, wazima katika imani na katika upendo na katika saburi. Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema; ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao; na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe. Vivyo hivyo na vijana waume uwaonye kuwa na kiasi; katika mambo yote ukijionyesha wewe mwenyewe kuwa kielelezo cha matendo mema, na katika mafundisho yako ukionyesha usahihi na ustahivu, na maneno yenye uzima yasiyoweza kuhukumiwa makosa, ili yule mwenye kupinga atahayarike, kwa kuwa hana neno baya la kunena juu yetu. Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa; tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu; ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema.

Wimbo wa Katikati

Zab 37:3-4, 18, 23, 27, 29

Umtumaini Bwana ukatende mema,
Ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu.
Nawe utajifurahisha kwa Bwana,
Naye atakupa haja za moyo wako.
(K) Wokovu wa wenye haki una Bwana

Bwana anazijua siku za wakamilifu,
Na urithi wao utakuwa wa milele.
Hatua za mtu zaimarishwa na Bwana,
Naye aipenda njia yake.
(K) Wokovu wa wenye haki una Bwana

Jiepue na uovu, utende mema,
Na kukaa hata milele.
Wenye haki watairithi nchi,
Nao watakaa humo milele.
(K) Wokovu wa wenye haki una Bwana

Injili

Lk 17:7-10

Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Ni nani kwenu mwenye mtumwa alimaye au achungaye ng'ombe, atakayemwambia mara arudipo kutoka shambani, Njoo upesi, keti, ule chakula? Je! Hatamwambia, Nifanyie tayari chakula, nile; jifunge unitumikie, hata niishe kula na kunywa, ndipo nawe utakapokula na kunywa? Je! Atampa asante yule mtumwa, kwa sababu ameyafanya aliyoagizwa? Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya.

Maoni


Ingia utoe maoni