Masomo ya Misa
Sikukuu ya Kung’ara Bwana Wetu Yesu Kristu (Jumapili, Agosti 06, 2023)
Dan 7:9-10, 13-14
Mimi nilitazama hata viti vya enzi vikawekwa, na mmoja aliye mzee wa siku ameketi; mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji, na nywele za kichwa chake kama sufu safi; kiti chake cha enzi kilikuwa miali ya moto, na gurudumu zake moto uwakao. Mto kama wa moto ukatoka ukapita mbele zake; maelfu elfu wakamtumikia, na elfu kumi mara elfu kumi wakasimama mbele zake; hukumu ikawekwa, na vitabu vikafunuliwa. Nikaona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu nave. Nave akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo haitapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa.
Zab 97:1-2, 5-6, 9
Bwana ametamalaki, nchi na ishangilie,
Visiwa vingi na vifurahi.
Mawingu na giza vyamzunguka,
Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake.
(K) Bwana ametamalaki, juu sana kuliko nchi yote.
Milima iliyeyuka kama nta mbele za Bwana,
Mbele za Bwana wa dunia yote.
Mbingu zimetangaza haki yake,
Na watu wote wameuona utukufu wake.
(K) Bwana ametamalaki, juu sana kuliko nchi yote.
Maana Wewe, Bwana, ndiwe Uliye juu,
Juu sana kuliko nchi yote;
Umetukuka sana juu ya miungu yote.
(K) Bwana ametamalaki, juu sana kuliko nchi yote.
2Pet 1:16-19
Hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, tulipowajulisha ninyi nguvu zake Bwana wetu Yesu Kristo na kuja kwake; bali tulikuwa tumeuona wenyewe ukuu wake. Maana alipata kwa Mungu Baba heshima na utukufu, hapo alipoletewa sauti iliyotoka katika utukufu mkuu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Na sauti hiyo sisi tuliisikia ikitoka mbinguni tulipokuwa pamoja naye katika mlima ule mtakatifu. Nasi tuna lile neno la unabii lililo imara zaidi, ambalo, mkiliangalia, kama taa ing’aayo mahali penye giza, mwafanya vyema, mpaka kutakapopambazuka, na nyota ya asubuhi kuzuka mioyoni mwenu.
Mt 17:5
Aleluya, aleluya,
Huyu ni mwanangu, mpendwa wangu,
ninayependezwa naye, msikieni yeye.
Aleluya.
Mt 17:1-9
Yesu aliwatwaa Petro, na Yakobo, na Yohane nduguye, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani; akageuka sura yake mbele yao; uso wake ukang’aa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama nuru. Na tazama, wakatokewa na Musa na Eliya, wakizungumza naye. Petro akajibu akamwambia Yesu, Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa; ukitaka, nitafanya hapa vibanda vitatu, kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya. Alipokuwa katika kusema, tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama sauti ikatoka katika lile wingu, ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye. Na wale wanafunzi waliposikia, walianguka kifulifuli, wakaogopa sana. Yesu akaja, akawagusa, akasema, Inukeni, wala msio- gope. Wakainua macho yao, wasione mtu ila Yesu peke yake. Na walipokuwa wakishuka mlimani, Yesu aliwaagiza, akasema, Msimwambie mtu ye yote habari ya maono hayo, hata Mwana wa Adamu atakapofufuka katika wafu.
Maoni
Ingia utoe maoni