Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Ijumaa ya 16 ya Mwaka (Ijumaa, Julai 28, 2023)  

Somo la 1

Kut 20:1-17

Mungu alinena maneno haya yote akasema, Mimi ni Bwana, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa. Usiwe na miungu ila mimi. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu. Usilitaje bure jina la Bwanu, mungu wako, maana Bwana hatamhesabia kuwa hana hatia mtu alitajaye jina lake bure. Ikumbuke siku ya sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni sabato ya Bwana, Mungu wako, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. Maana, kwa siku sita Bwana alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba; kwa hiyo Bwana akaibarikia siku ya sabato akaitakasa. Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana. Mungu wako. Usiue. Usizini. Usiibe. Usimshuhudie jirani yako uongo. Usiitamani nyumba ya jirani yako, usimtamani mke wa jirani yako; wala mtumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng’ombe wake, wala punda wake, wala cho chote alicho nacho jirani yako.

Wimbo wa Katikati

Zab 19:8-11

Sheria ya Bwana ni kamilifu huiburudisha nafsi
Ushuhuda wa Bwana ni amini humtia mjinga hekima.
(K) Bwana, unayo maneno ya uzima wa milele.

Maagizo ya Bwana ni adili, huufurahisha moyo,
Amri ya Bwana ni safi, huyatia macho nuru.
(K) Bwana, unayo maneno ya uzima wa milele.

Kicho cha Bwana ni kitakatifu, kinadumu milele.
hukumu za Bwana ni kweli, zina haki kabisa.
(K) Bwana, unayo maneno ya uzima wa milele.

Ni za kutamanika kuliko dhahabu,
kuliko wingi wa dhahabu safi.
Nazo ni tamu kuliko asali, kuliko sega la asali.
(K) Bwana, unayo maneno ya uzima wa milele.

Shangilio

Mt 4:4

Aleluya, aleluya,
Mtu hataishi kwa mkate tu,
ila kwa kila neno litokalo
katika kinywa cha Mungu
Aleluya.

Injili

Mt 13:18-23

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ninyi sikilizeni mfano wa mpanzi. Kila mtu alisikiapo neno la ufalme asielewe nalo, huja yule mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake. Huyo ndiye aliyepandwa karibu na njia. Naye aliyepandwa penye miamba. huyo ndiye alisikiaye lile neno, akalipokea mara kwa furaha; lakini hana mizizi ndani yake, bali hudumu kwa muda; ikitukia dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara huchukizwa. Naye aliyepandwa penye miiba, huyo ndiye alisikiaye lile neno; na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno; likawa halizai. Naye aliyepandwa penye udongo mzuri, huyo ndiye alisikiaye lile neno, na kuelewa nalo; yeye ndiye azaaye matunda, huyu mia, na huyu sitini, na huyu thelathini.

Maoni


Ingia utoe maoni