Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumamosi ya 16 ya Mwaka (Jumamosi, Julai 29, 2023)  

Somo la 1

Kut 24:3-8

Musa aliwambia watu maneno yote ya Bwana, na hukumu zake zote; watu wote wakajibu kwa sauti moja, wakasema, Maneno yote aliyoyanena Bwana tutayatenda. Basi Musa akayaandika maneno yote ya Bwana, akaondoka asubuhi na mapema, akajenga madhabahu chini ya mlima, na nguzo kumi na mbili, kwa hesabu ya kabila kumi na mbili za Israeli, akapeleka vijana wa wana wa Israeli, waliotoa sadaka za kuteketezwa, wakamchinjia Bwana sadaka za amani za ng’ombe. Musa akatwaa nusu ya ile damu, akaitia katika mabakuli; na nusu ya ile damu akainyunyiza juu ya madhabahu. Kisha akakitwaa kitabu cha agano akakisoma masikioni mwa watu; wakasema, Hayo yote aliyoyanena Bwana tutayatenda, nasi tutatii. Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyizia watu, akasema, Hii ndiyo damu ya agano alilolifanya Bwana pamoja nanyi katika maneno haya yote.

Wimbo wa Katikati

Zab 50:1-2, 5-6, 14-15

Mungu, Mungu Bwana, amenena, ameiita nchi,
Toka maawio ya jua hata machweo yake.
Tokea Sayuni,, ukamilifu wa uzuri,
Mungu amemulika.
(K) Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru.

Nikusanyieni wacha Mungu wangu,
Waliofanya agano nami kwa dhabihu.
Na mbingu zitatangaza haki yake,
Kwa maana Mungu ndiye aliye hakimu.
(K) Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru.

Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru;
Mtimizie Aliye juu nadhiri zako.
Ukaniite siku ya mateso;
Nitakuokoa, na wewe utanitukuza.
(K) Mtolee Mungu dhabihu za kushukuru.

Shangilio

Zab 8:15

Aleluya, aleluya,
Wanabarikiwa wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao, hulisikia neno la Mungu na kulishika.
Aleluya.

Injili

Mt 13:24–30

Yesu aliwatolea makutano mfano akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake; lakini watu walipolala akaja adui yake akapanda magugu katikati ya agano, akaenda zake. Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu. Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu? Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye? Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo. Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu.

Maoni


Ingia utoe maoni