Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumatatu ya 16 ya Mwaka (Jumatatu, Julai 24, 2023)  

Somo la 1

Kut 14:5-18

Mfalme wa Misri aliambiwa ya kuwa wale watu wamekwisha kimbia; na moyo wa Farao, na mioyo ya watumishi wake, iligeuzwa iwe kinyume cha hao watu, nao wakasema, Ni nini jambo hili tulilotenda, kwa kuwaacha Waisraeli waende zao wasitutumikie tena? Akaandalia gari lake, akawachukua watu wake pamoja naye; tena akatwaa magari mia sita yaliyochaguliwa, na magari vote ya Misri, na maakida juu ya magari hayo vote. Na Bwana akaufanya moyo wake Farao mfalme wa Misri kuwa mgumu, naye akawafuata wana wa Israeli; kwa sababu wana wa Israeli walitoka kwa ujeuri. Wamisri wakafuata nyuma yao, farasi zote na magari yote ya Farao, na askari zake wenye kupanda farasi, na jeshi lake, nao wakawapata hali wamepanga pale karibu na bahari, karibu na Pi-hahirothi, kukabili Baal-sefoni. Hata Farao alipokaribia, wana wa Israeli wakainua macho yao, na tazama, Wamisri wanakuja nyuma yao; wakaogopa sana; wana wa Israeli wakamlilia Bwana. Wakamwambia Musa, Je! kwa sababu hapakuwa na makaburi katika Misri umetutoa huko ili tufe jangwani? Mbona umetutendea haya, kututoa katika nchi ya Misri? Neno hili silo tulilokuambia huko Misri, tukisema, Tuache tuwatumikie Wamisri? Maana ni afadhali kuwatumikia Wamisri kuliko kufa jangwani. Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa Bwana atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. Bwana atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya. Bwana akamwambia Musa, Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele. Nawe inua fimbo yako, ukanyoshe mkono wako juu ya bahari, na kuigawanya; nao wana wa Israeli watapita kati ya bahari katika nchi kavu. Nami, tazama, nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu, nao wataingia na kuwafuatia, nami nitajipatia utukufu kwa Farao, na kwa jeshi lake lote, kwa magari yake na kwa wapanda farasi wake. Na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapokwisha kujipatia utukufu kwa Farao, na magari yake, na farasi zake.

Wimbo wa Katikati

Kut 15:1-6

Nitamwimbia Bwana, kwa maana ametukuka sana;
Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini.
Bwana ni nguvu zangu, na wimbo wangu;
Naye amekuwa wokovu wangu.
Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu;
Ni Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza.
(K) Nitamwimbia Bwana, kwa maana ametukuka sana.

Bwana ni mtu wa vita,
Bwana ndilo jina lake.
Magari ya Farao na jeshi lake amewatupa baharini,
Maakida yake wateule wamezama katika bahari ya Shamu.
(K) Nitamwimbia Bwana, kwa maana ametukuka sana.

Vilindi vimewafunikiza,
Walizama vilindini kama jiwe.
Bwana, mkono wako wa kuume
umepata fahari ya uwezo,
Bwana, mkono wako wa kuume wawasetaseta adui.
(K) Nitamwimbia Bwana, kwa maana ametukuka sana.

Shangilio

Yn 15:15

Aleluya, aleluya,
Bwana anasema: Siwaiti tena watumwa,
lakini ninyi nimewaita rafiki,
kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.
Aleluya.

Injili

Mt 12:38-42

Baadhi ya waandishi wa Mafarisayo walimjibu Yesu wakasema, Mwalimu, twataka kuona ishara kwako. Akajibu, akawaambia, Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya nabii Yona. Kwani kama vile Yona alivyokuwa siku tatu mchana na usiku katika tumbo la nyangumi, hivyo ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa siku tatu mchana na usiku katika moyo wa nchi. Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, nao watawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona; na hapa yupo aliye mkuu kuliko Yona. Malkia wa kusini atasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu yeye alikuja kutoka pande za mwisho za dunia ili asikie hekima ya Sulemani, na hapa yupo aliye mkuu kuliko Sulemani.

Maoni


Ingia utoe maoni