Masomo ya Misa
Sikukuu ya Mt. Yakobo, Mtume (Jumanne, Julai 25, 2023)
2Kor 4:7-15
Tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu. Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa; twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi; siku zote twachukua katika mwili kuuawa kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu. Kwa maana sisi tulio hai, siku zote twatolewa tufe kwa ajili ya Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu ipatikanayo na mauti. Basi hapo mauti hufanya kazi ndani yetu, bali uzima ndani yenu. Lakini kwa kuwa tuna roho ile ile ya imani; kama ilivyoandikwa, Naliamini, na kwa sababu hiyo nalinena; sisi nasi twaamini, na kwa sababu hiyo twanena; tukijua ya kwamba yeye aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi nasi pamoja na Yesu, na kutuhudhurisha pamoja nanyi. Kwa maana mambo yote ni kwa ajili yenu, ili neema hiyo ikiongezwa sana, kwa hao walio wengi shukrani izidishwe, na Mungu atukuzwe.
Zab 126
Bwana alipowarejeza mateka wa Sayuni,
Tulikuwa kama waotao ndoto.
Ndipo kinywa chetu kilipojaa kicheko,
Na ulimi wetu kelele za furaha.
(K) Wapandao kwa machozi watavuna kwa kelele za furaha
Ndipo waliposema katika mataifa,
Bwana amewatendea mambo makuu.
Bwana alitutendea mambo makuu,
Tulikuwa tukifurahi.
(K) Wapandao kwa machozi watavuna kwa kelele za furaha
Ee Bwana, uwarejeze watu wetu waliofungwa,
Kama vijito vya Kusini.
Wapandao kwa machozi Watavuna kwa kelele za furaha.
(K) Wapandao kwa machozi watavuna kwa kelele za furaha
Ingawa mtu anakwenda zake akilia,
Azichukuapo mbegu za kupanda.
Hakika atarudi kwa kelele za furaha,
Aichukuapo miganda yake.
(K) Wapandao kwa machozi watavuna kwa kelele za furaha
Yn 15:16
Aleluya, aleluya
Ni mimi niliyewachagua ninyi nikawaweka mwende mkazae matunda, na matunda yenu yapate kukaa, asema Bwana
Aleluya
Mt 20:20-28
Mama yao wana wa Zebedayo akamwendea pamoja na wanawe, akamsujudia, na kumwomba neno. Akamwambia, Wataka nini? Akamwambia, Agiza kwamba hawa wanangu wawili waketi mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika ufalme wako. Yesu akajibu akasema, Hamjui mnaloliomba. Je! Mwaweza kunywea kikombe nitakachonywea mimi? Wakamwambia, Twaweza. Akawaambia, Hakika mtakinywea kikombe changu; lakini kuketi mkono wangu wa kuume na mkono wangu wa kushoto, sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na Baba yangu. Na wale kumi waliposikia, waliwakasirikia wale ndugu wawili. Lakini Yesu akawaita, akasema, Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu ye yote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; na mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.
Maoni
Ingia utoe maoni