Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumamosi ya 8 ya Mwaka (Jumamosi, Juni 03, 2023)  

Somo la 1

YbS 51:12-20

Wapenzi, nitamshukuru na kumsifu, na kulihimidi Jina la Bwana. Mimi nilipokuwa kijana, kabla sijasafiri bado, naliitafuta hekima kwa bidii katika sala yangu, na mbele ya hekalu nikaomba, nami hata mwisho nitazidi kuitafuta. Ikachanua kama zabibu inavyoiva, na moyo wangu ukapendezwa, na mguu wangu ukaenda katika njia iliyo sawa. Tangu ujana wangu nikafanya kuaua, nikaliinamisha sikio kidogo, nikaipokea, nikajipatia mafundisho tele. Kwangu nira yake ikawa utukufu, nami nitamshukuru Yeye aliyenifundisha. Kwa maana nalikusudi kujizoeza nayo, nikajitahidi katika yaliyo mema, wala sitatahayarishwa. Roho yangu imeshindana kwa nguvu ndani yake, na mintarafu kutenda kwangu nalikuwa mwangalifu; nikainyosha mikono yangu juu mbinguni, nikaulalamikia ujinga wangu. Nikaielekeza roho yangu moja kwa moja kwake, na katika unyofu nikaiona; tangu mwanzo nikajipatia ufahamu, na kwa hiyo sitakataliwa milele.

Wimbo wa Katikati

Zab 19 : 7-11

Sheria ya Bwana ni kamilifu,
Huiburudisha nafsi.
Ushuhuda wa Bwana ni amini,
Humtia mjinga hekima.
(K) Amri ya Bwana anafurahisha moyo.

Maagizo ya Bwana ni ya adili,
Huufurahisha moyo.
Amri ya Bwana ni safi,
Huyatia macho nuru.
(K) Amri ya Bwana anafurahisha moyo.

Kicho cha Bwana ni kitakatifu,
Kinadumu milele.
Hukumu za Bwana ni kweli,
Zina haki kabisa.
(K) Amri ya Bwana anafurahisha moyo.

Ni za kutamanika kuliko dhahabu,
Kuliko wingi wa dhahabu safi.
Nazo ni tamu kuliko asali,
Kuliko sega la asali.
(K) Amri ya Bwana anafurahisha moyo.

Shangilio

Zab 119:18

Aleluya, aleluya,
Unifumbue macho yangu niyatazame, maajabu yatokayo katika sheria yako.
Aleluya.

Injili

Mk 11:27-33

Yesu na wanafunzi walifika Yerusalemu; alipokuwa akitembea hekaluni, walimwendea wakuu wa makuhani, na waandishi, na wazee, wakamwambia, Ni kwa mamlaka gani unatenda mambo haya? naye ni nani aliyekupa mamlaka hii uyatende haya? Yesu akawaambia, Nitawauliza neno moja, nanyi mnijibu, kisha nitawaambia ni kwa mamlaka gani nayatenda haya. Ubatizo wa Yohane ulitoka mbinguni, au kwa wanadamu? Nijibuni. Wakasemezana wao kwa wao, wakisema, Kama tukisema, Ulitoka mbinguni, atasema, Mbona, basi, hamkumwamini? Ila tukisema, Ulitoka kwa wanadamu. Waliogopa watu; maana watu wote walimwona Yohane kuwa nabii halisi. Wakamjibu Yesu, wakasema, Hatujui. Yesu akawaambia, Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa mamlaka gani nayatenda haya.

Maoni


Ingia utoe maoni