Alhamisi. 18 Aprili. 2024

Masomo ya Misa

Ijumaa ya 34 ya Mwaka (Ijumaa, Novemba 25, 2022)  

Somo la 1

Ufu 20:1-4, 11-21:2

Mimi, Yohane, niliona malaika akishuka kutoka mbinguni, mwenye ufunguo wa kuzimu, na mnyororo mkubwa mkononi mwake. Akamshika yule joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ni Ibilisi na Shetani, akamfunga miaka elfu; akamtupa katika kuzimu, akamfunga, akatia muhuri juu yake, asipate kuwadanganya mataifa tena, hata ile miaka elfu itimie; na baada ya hayo yapasa afunguliwe muda mchache. Kisha nikaona viti vya enzi, wakaketi juu yake, nao wakapewa hukumu; nami nikaona roho zao waliokatwa vichwa kwa ajili ya ushuhuda wa Yesu, na kwa ajili ya neno la Mungu, na hao wasiomsujudia yule mnyama, wala sanamu yake, wala hawakuipokea ile chapa katika vipaji vya nyuso zao, wala katika mikono yao; nao wakawa hai, wakatawala pamoja na Kristo miaka elfu. Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana. Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao. Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto. Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya; kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza zimekwisha kupita, wala hapana bahari tena. Nami nikauona mji ule mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, umewekwa tayari, kama bibi-arusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe.

Wimbo wa Katikati

Zab 84:2-5, 7

Nafsi yangu imezionea shauku nyua za Bwana,
Naam, na kuzikondea. Moyo wangu na mwili wangu Vinamlilia Mungu aliye hai.
(K) Mungu anakuwa pamoja na watu

Shomoro naye ameona nyumba, Na mbayuwayu amejipatia kioto,
Alipoweka makinda yake, Kwenye madhabahu zako,
Ee Bwana wa majeshi, Mfalme wangu na Mungu wangu.
(K) Mungu anakuwa pamoja na watu

Heri wakaao nyumbani mwako,
Wanakuhimidi daima.
Heri ambaye nguvu zake zatoka kwako,
(K) Mungu anakuwa pamoja na watu

Huendelea toka nguvu hata nguvu,
Huonekana Sayuni kila mmoja mbele za Mungu.
(K) Mungu anakuwa pamoja na watu

Shangilio

Zab 19:8

Aleluya, aleluya,
Amri ya Bwana ni safi, huyatia macho nuru.
Aleluya.

Injili

Lk 21:29-33

Yesu aliwaambia wanafunzi wake mfano; Utazameni mtini na miti mingine yote. Wakati iishapo kuchipuka, mwaona na kutambua wenyewe ya kwamba majira ya mavuno yamekwisha kuwa karibu. Nanyi kadhalika, mwonapo mambo hayo yanaanza kutokea, tambueni ya kwamba ufalme wa Mungu u karibu. Amin, nawaambieni, Kizazi hiki hakitapita hata hayo yote yatimie. Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.

Maoni


Ingia utoe maoni