Masomo ya Misa
Dominika ya 7 ya Mwaka (Jumapili, Februari 20, 2022)
1Sam 26:2, 7-9, 12-13, 22-23
Sauli aliondoka, akashuka nyikani kwa Zifu, naye alikuwa na watu elfu tatu, wateule wa Israeli, pamoja naye, ili kumtafuta Daudi katika nyika ya Zifu. Basi Daudi na Abishai wakawaendea watu usiku; na tazama, Sauli alikuwapo kati ya magari amelala usingizi, na fumo lake limechomekwa chini, karibu na kichwa chake; naye Abneri na watu wake wamelala wakimzunguka. Ndipo Abishai akamwambia Daudi, Mungu amemtia adui yako mikononi mwako leo; basi, niache nimpige kwa hilo fumo hata nchi kwa pigo moja, sitampiga mara ya pili. Lakini Daudi akamwambia Abishai, Usimwangamize; kwani ni nani awezaye kuunyosha mkono wake juu ya masihi. Basi Daudi akalitwaa lile fumo, na lile gudulia la maji, kichwani pa Sauli; nao wakaenda zao, wala hapana mtu aliyeliona jambo hili wala kulijua, wala kuamka; maana wote walikuwa wamelala; kwa kuwa usingizi mzito kutoka kwa Bwana umewaangukia. Kisha Daudi akaenda ng'ambo ya pili, akasimama juu ya kilima, mbali sana; palipokuwapo nafasi tele katikati yao; Daudi akajibu, akasema, Litazame fumo hili, Ee mfalme! Kijana mmoja na avukie huku, alitwae. Naye Bwana atamlipa kila mtu haki yake, na uaminifu wake; maana Bwana amekutia mikononi mwangu leo, nami nalikataa kuunyosha mkono wangu juu ya masihi wa Bwana.
Zab 103:1-4, 8, 10, 12-13
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
Naam, vyote vilivyo ndani yangu Vilihimidi jina lake takatifu.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Wala usizisahau fadhili zake zote.
(K) Bwana amejaa huruma na neema.
Akusamehe maovu yako yote,
Akuponya magonjwa yako yote,
Aukomboa uhai wako na kaburi,
Akutia taji ya fadhili na rehema.
(K) Bwana amejaa huruma na neema.
Bwana amejaa huruma na neema,
Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili.
Hakututenda sawasawa na hatia zetu,
Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu.
(K) Bwana amejaa huruma na neema.
Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi,
Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi.
Kama vile baba awahurumiavyo watoto wake,
Ndivyo Bwana anavyowahurumia wamchao.
(K) Bwana amejaa huruma na neema.
1Kor 15:45-49
Ndivyo ilivyoandikwa, Mtu wa kwanza, Adamu, akawa nafsi iliyo hai; Adamu wa mwisho ni roho yenye kuhuisha. Lakini hautangulii ule wa roho, bali ule wa asili; baadaye huja ule wa roho. Mtu wa kwanza atoka katika nchi, ni wa udongo. Mtu wa pili atoka mbinguni. Kama alivyo yeye wa udongo, ndivyo walivyo walio wa udongo; na kama alivyo yeye wa mbinguni, ndivyo walivyo walio wa mbinguni. Na kama tulivyoichukua sura yake yule wa udongo, kadhalika tutaichukua sura yake yeye aliye wa mbinguni.
Yn 13:34
Aleluya, aleluya
Nawapa amri mpya, mpendane, Kama vile nilivyowapenda ninyi, Nanyi mpendane vivyo hivyo.
Aleluya.
Lk 6:27-38
Siku ile Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Nawaambia ninyi mnaosikia, Wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi, wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi. Akupigaye shavu moja, mgeuzie la pili, naye akunyang'anyaye joho yako, usimzuilie na kanzu. Mpe kila akuombaye, na akunyang'anyaye vitu vyako, usitake akurudishie. Na kama mnavyotaka watu wawatendee ninyi, watendeeni vivyo hivyo. Maana mkiwapenda wale wawapendao ninyi, mwaonyesha fadhili gani? Kwa kuwa hata wenye dhambi huwapenda wale wawapendao. Nanyi mkiwatendea mema wale wawatendeao mema, mwaonyesha fadhili gani? Hata wenye dhambi hufanya vivyo hivyo. Na mkiwakopesha watu huku mkitumaini kupata kitu kwao, mwaonyesha fadhili gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi, ili warudishiwe vile vile. Bali wapendeni adui zenu, tendeni mema, na kukopesha msitumaini kupata malipo, na thawabu yenu itakuwa nyingi; nanyi mtakuwa wana wa Aliye juu, kwa kuwa yeye ni mwema kwa wasiomshukuru, na waovu. Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma. Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa. Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.
Maoni
Ingia utoe maoni