Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumamosi ya 6 ya Mwaka (Jumamosi, Februari 19, 2022)  

Somo la 1

Yak 3:1-10

Ndugu zangu, msiwe waalimu wengi, mkijua ya kuwa mtapata hukumu kubwa zaidi. Maana twajikwaa sisi sote pia katika mambo mengi. Mtu asiyejikwaa katika kunena, huyo ni mtu mkamilifu, awezaye kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu. Angalieni, twatia lijamu katika vinywa vya farasi, ili wamtii, hivi twageuza mwili wao wote. Tena angalieni merikebu; ingawa ni kubwa kama nini, na kuchukuliwa na pepo kali, zageuzwa na usukani mdogo sana, ko kote anakoazimia kwenda nahodha. Vivyo hivyo ulimi nao ni kiungo kidogo, nao hujivuna majivuno makuu. Angalieni jinsi moto mdogo uwashavyo msitu mkubwa sana. Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfulizo wa maumbile, nao huwashwa moto na jehanum. Maana kila aina ya wanyama, na ya ndege, na ya vitambaavyo, na ya vitu vilivyomo baharini, vinafugika, navyo vimekwisha kufugwa na wanadamu. Bali ulimi hakuna awezaye kuufuga; ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti. Kwa huo twamhimidi Mungu Baba yetu, na kwa huo twawalaani wanadamu waliofanywa kwa mfano wa Mungu. Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo.

Wimbo wa Katikati

Zab 12:2-3, 4-5, 7-8

Bwana, uokoe, maana mcha Mungu amekoma,
Maana waaminifu wametoweka katika wanadamu.
Husemezana yasiyofaa kila mtu na mwenziwe,
Wenye midomo ya kujipendekeza;
Husemezana kwa mioyo ya unafiki;
(K) Wewe, Bwana ndiwe utakayetuhifadhi.

Bwana ataikata midomo yote ya kujipendekeza,
Nao ulimi unenao maneno ya kiburi;
Waliosema, Kwa ndimi zetu tutashinda;
Midomo yetu ni yetu wenyewe,
Ni nani aliye bwana juu yetu?
(K) Wewe, Bwana ndiwe utakayetuhifadhi.

Maneno ya Bwana ni maneno safi,
Ni fedha iliyojaribiwa kalibuni juu ya nchi;
Iliyosafishwa mara saba.
Wewe, Bwana, ndiwe utakayetuhifadhi,
Utatulinda na kizazi hiki milele.
(K) Wewe, Bwana ndiwe utakayetuhifadhi.

Injili

Mk 9:2-13

Siku ile Yesu aliwatwaa Petro, na Yakobo, na Yohana, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani, peke yao; akageuka sura yake mbele yao; mavazi yake yakimeta-meta, meupe mno, jinsi asivyoweza dobi duniani kuyafanya meupe. Wakatokewa na Eliya pamoja na Musa, nao walikuwa wakizungumza na Yesu. Petro akajibu, akamwambia Yesu, Rabi, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu, kimoja chako wewe, kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya. Maana, hakujua la kunena, kwa kuwa waliingiwa na hofu nyingi. Kisha likatokea wingu, likawatia uvuli; sauti ikatoka katika lile wingu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye. Mara hiyo walipotazama huku na huku, hawakuona mtu pamoja nao ila Yesu peke yake. Na walipokuwa wakishuka mlimani aliwakataza wasimweleze mtu waliyoyaona, hata Mwana wa Adamu atakapokuwa amefufuka katika wafu. Wakalishika neno lile, wakiulizana wao kwa wao, Huko kufufuka katika wafu maana yake nini? Wakamwuliza, wakisema, Mbona waandishi hunena ya kwamba imempasa Eliya kuja kwanza? Akajibu akawaambia, Ni kweli Eliya yuaja kwanza, na kurejeza upya yote; lakini, pamoja na haya, ameandikiwaje Mwana wa Adamu ya kwamba atateswa mengi na kudharauliwa? Lakini nawaambia, Eliya amekwisha kuja, nao wakamtenda yote waliyoyataka kama alivyoandikiwa.

Maoni

Deograsias Haule

Muwe mnaandika na masomo ya siku inayofuata.

Ingia utoe maoni