Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 4 ya Mwaka (Jumapili, Januari 30, 2022)  

Somo la 1

Yer 1:4-5, 17-19

Neno la Bwana lilinijia, kusema, Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa. Haya basi, wewe jifunge viuno, ukaondoke ukawaambie maneno yote niliyokuamuru; usifadhaike kwa ajili yao, nisije nikakufadhaisha wewe mbele yao. Maana, tazama, nimekufanya leo kuwa mji wenye boma, na nguzo ya chuma, na kuta za shaba, juu ya nchi yote; juu ya wafalme wa Yuda, na juu ya wakuu wake, na juu ya makuhani wake, na juu ya watu wa nchi hii. Nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, asema Bwana, ili nikuokoe.

Wimbo wa Katikati

Zab 71:1-2, 3-4, 4-6, 15-17

Nimekukimbilia Wewe, Bwana,
Nisiaibike milele.
Kwa haki yako uniponye, uniopoe,
Unitegee sikio lako, uniokoe.
(K) Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako.

Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu,
Nitakakokwenda sikuzote.
Umeamuru niokolewe,
Ndiwe genge langu na ngome yangu.
Ee Mungu wangu, uniopoe mkononi mwa mkorofi,
(K) Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako.

Katika mkono wake mwovu, mdhalimu,
Maana ndiwe taraja langu, Ee Bwana MUNGU,
Tumaini langu tokea ujana wangu.
Nimekutegemea Wewe tangu kuzaliwa,
Ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu,
Ninakusifu Wewe daima.
(K) Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako.

Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako Mchana kutwa; maana sijui hesabu yake.
Nitakuja na mambo ya ajabu ya Bwana MUNGU;
Nitawakumbusha watu haki yako Wewe peke yako.
Ee Mungu, umenifundisha tokea ujana wangu;
Nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata leo.
(K) Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako.

Somo la 2

1Kor 12:31; 13:1-13

Takeni sana karama zilizo kuu. Hata hivyo nawaonyesha njia iliyo bora. Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao. Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi. Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu. Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote. Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika. Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu; lakini ijapo ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabatilika. Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto. Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana. Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo.

Shangilio

Efe 1:17,18

Aleluya, aleluya
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika mkujua yeye. Macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo, na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo
Aleluya

Injili

Lk 4:21-30

Yesu aliwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu. Wakamshuhudia wote, wakiyastaajabia maneno ya neema yaliyotoka kinywani mwake, wakasema, Huyu siye mwana wa Yusufu? Akawaambia, Hapana shaka mtaniambia mithali hii, Tabibu, jiponye nafsi yako; mambo yote tuliyosikia kwamba yametendeka Kapernaumu, yatende na hapa pia katika nchi yako mwenyewe. Akasema, Amin, nawaambia ya kwamba, Hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe. Lakini, kwa hakika nawaambia, Palikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli zamani za Eliya, wakati mbingu zilipofungwa miaka mitatu na miezi sita, njaa kuu ikaingia nchi nzima; wala Eliya hakutumwa kwa mmojawapo, ila kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni. Tena, palikuwa na wenye ukoma wengi katika Israeli zamani za nabii Elisha, wala hapana aliyetakaswa ila Naamani, mtu wa Shamu. Wakajaa ghadhabu wote waliokuwa katika sinagogi walipoyasikia hayo. Wakaondoka wakamtoa nje ya mji, wakampeleka mpaka ukingo wa kilima ambacho mji wao umejengwa juu yake, wapate kumtupa chini; lakini yeye alipita katikati yao, akaenda zake.

Maoni


Ingia utoe maoni