Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Januari 30, 2022

Ndugu wapendwa karibuni kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ambapo ni Dominika ya 4 ya mwaka C wa kanisa. Ujumbe wa neno la Mungu leo unatualika kumtumainia Bwana. Hakika maishani utakutana na magumu mazito, yatakuja kwa kasi sana na kukuogopesha kweli. Yatakuvamia na kukutishia lakini yabidi tumkimbilie Bwana na ndiye atakayetuokoa. Ndio ujumbe mkuu tunaokutana nao ndugu zangu.

Zaburi yetu ya wimbo wa katikati, Zaburi ya 71 inatualika vyema kutafakari ujumbe huu. Maneno ya zaburi hii yanasema midomo yangu itasimulia juu ya wema wako. Mwimbaji anamualika Mungu amlinde, awe kwake mwamba wa usalama na hakika asimuache. Zaburi hii ni sala iliyosaliwa na mzee aliyekuwa na umri mkubwa lakini alikuwa akihangaishwa na maadui wengi sana katika huu uzee wake. Mzee huyu alikuwa na imani, alijua kwamba aliwahi kusaidiwa na Bwana alipomlilia. Hivyo kwa kipindi hiki, hakika Bwana hatamuacha tena. Bwana atamsaidia tu.

Daudi alitumia zaburi hii kumwomba Mungu aliposhambuliwa na mtoto wake Absalomu aliyepindua utawala wake na kutaka kumuua. Daudi alimlia Mungu na kumweleza kwamba ee Bwana, uliwahi kunikinga na akina Goliathi, na akina Sauli-hivyo basi nikinge na huyu adui mwingine. Kweli Bwana alimkinga na kuweza kumshinda Absalomu. Zaburi hii inatualika na sisi pia kumlilia Bwana kwa matumaini, tukumbushie ukuu wake na wema wake aliowahi kututendea na hivi viwe kwa ajili ya kutuletea matumaini ya kuzidi kusali na kumtumainia Mungu.

Kwenye somo la kwanza tunakutana na Mungu akimuitia nabii Yeremia na kumtia Moyo. Nabii Yeremia alitoka familia ya kimaskini, anaitwa akawatolee unabii-kuwakemea na kuwaonya wafalme wa Yuda. Yeye anaogopa anasema siwezi, mimi ninaumri mdogo na siwezi kusema kuwashawishi hawa wakuu wa Yuda. Mungu anamueleza kwamba usifikiri kwamba ati sikujui, mimi ninakufahamu zaidi ya unavyojifahamu wewe, nilishakutakasa kabla hujazaliwa na ninafahamu kwamba unaweza. Wewe endelea kunitumainia, nitakutia nguvu ya kuweza kupambana nao. Lakini ukiogopa tu, umekwisha.

Maneno haya yalimsaidia Yeremia kupambana na uadui mgumu wa wana wa Yuda. Alikamatwa na kuchapwa viboko, akafungwa gerezani, akachukiwa na kila mtu, akapigwa na kutupwa shimoni. Kati ya manabii walioteswa na wafalme wa Israeli mmojawapo alikuwa Yeremia. Aliteseka sana. Lakini hakushindwa au kukata tamaa. Hii nguvu aliyoipata hapa katika kuitwa kwake ilimsaidia sana kusonga mbele.

Naomba ndugu zangu tujifunze kitu toka kwa Yeremia. Kwanza, Mungu anatufahamu zaidi ya sisi tunavyojifahamu. Wengi wetu tunakwenda kumuelezea Mungu jinsi tulivyo lakini Mungu anatufahamu. Hivyo, akikuchagua kwa kazi yake, au kukupa majukumu yoyote-wewe jiamini-songa mbele-kama Yeremia asingalijiamini-hakika angalishindwa. Jiamini unaweza kwani Mungu amekwishasema unaweza.

Pili, Bwana anawafahamu wanadamu wake na alikwishawatakasa kabla ya kutungwa mimba. Tuwaheshimu vichanga. Kumetokea utamaduni wa kufikiri kwamba havina hadhi lakini Bwana anavifahamu, alikwishavitakasa, anajua hata unywele juu ya vichwa vyao. Hivyo tuache kuvionea.

Upo wakati tuliokwishakusaidiwa na Bwana, tukatembea na Bwana, tukauona wema wake. Nyakati hizo zitusaidie na kutupa imani kukabiliana na kipindi cha shida na changamoto. Tumweleze Mungu kwamba kipindi hiki ulitembea nasi vizuri sana. Tusaidie pia kwa kipindi hiki ee Mwenyezi Mungu.

Tuache kutaka kuhubiri yale tunayotaka kusikia. Utakuta mhubiri kama anataka pesa, ataitafuta namna ya kuingiza tu. Hapa ujumbe wako utakosa nguvu ya Mungu na hakika utashindwa tu kutoa chachu kwa watu.

Katika injili yetu, tunakutana na Yesu akienda kwa watu wa nyumbani mwake na huko hapokelewi vizuri. Kwa sababu alikuwa ni wa hapahapa tu, kutoka katika familia ya kimaskini. Wakakataa kumsikiliza, wakamwambia huna la kutuambia wewe kama baadhi ya wafalme wa Yuda walivyomwangalia Yeremia. Yesu anawaeleza ukweli kwamba ama kweli nabii hakubaliki katika mji wake; na kutokana na hilo, huwa watu wa nyumbani mwake hawafaidi. Wanafaidi wa nje tu. Anawaeleza kwamba hata enzi za mfalme Elisha anashangaa kuona kwamba walioponywa enzi za Elisha ni wageni-mtu wa Syria. Waisraeli waliachwa.

Kwanini? Kwa sababu walikuwa na imani kuliko waisraei wenyewe. Na hata Elia hakutumwa kwa Muisraeli ili amlishe bali alitumwa akalishwe na mama wa mataifa toka taifa la Sydoni. Kwa nini? Huyu mama alikuwa na imani. Mama wa kiisraeli angalikataa kumlisha na kushirikiana na Mungu vyema. Na nyie ni hivi hivi, mimi natumwa kwa wengine, wengine ndio watakaonifaidi. Sishangai kwamba mnanikataa na mimi pia, walikataliwa na manabii pia, mimi nasonga mbele kwa wengine na wao watafaidi zaidi.

Ndugu zangu, hapa tujifunze mambo makuu.

Kwanza, Mungu anahitaji imani. Imani inakufanya unashirikiana na Mungu na kumsaidia kutimiza kazi yake. Kama mama Maria au Yosefu angalikosa imani, Mungu asingalimtumia, tusingalibarikiwa hivi ndugu zangu. Sisi tuthamini imani. Mungu anafanya kazi na watu wenye imani. Tuwe makini, ukishakosa imani utashangaa unapitwa tu.
Imani inahitaji kujitoa kweli kwa bwana.

Tukitegemea kwamba tutakuwa watu wa kupata tu, hakika hatutakaa tuweze kutenda kazi yoyote ya Bwana. Yule mwanamke wa Serepta alikuwa tayari kupoteza unga wake na mafuta yake ili Elia apate kula na ndio Bwana akaweza kufanya naye kazi.

Hata na sisi, ili uweze kuwa padre-lazima ujitoe, sadaka kwa kazi ya Bwana. Ukisema kwamba uwe mtu wa kupata tu-hakika hutaweza kuwa padre na kufanya kazi ya Bwana. Hutaweza hata kuifanya. Hata kwenye ndoa-lazima ukubali kupoteza uweze kuishi huko kwenye ndoa yako. Na kama ilivyotokea kwa Maria. Hivyo, lazima tuwe watu wa kukubali kujitoa sadaka ili tuweze kutumiwa, tuwe watu wenye kukubali kupoteza ili tupate. Tukitegemea kwamba tutakuwa watu wa kupata tu, hakika hatutakaa tuweze kutenda kazi yoyote ya Bwana.

Dharau zinatukosesha mengi, zimetufanya tusiwasikilize baadhi ya watu, tukawaona kwamba wameishiwa, hawawezi kutuhubiria. Dharau hukufanya ukose imani, umuone kwamba hivi huyu kweli niliyemuona juzijuzi anaweza kuniambia kitu? Haka katoto nilichokazalisha juzi chaweza kumshusha Yesu na kumla-nakueleza ndugu zangu-anaweza, kuwa na imani. Dharau zitatuangusha, Mama Maria aliondoa dharau kabisa. Hata kama ni mtoto wake, alipiga magoti kumwabudu. Sisi tuwe namna hiyo ndugu zangu, tupige magoti hata kwa watoto zetu ndio unaweza kubarikiwa. Kwa mfano ukienda hospitalini, unakuta anayekuandikia dawa ni katoto cha miaka 24. Sasa kataa mwambie huwezi kunitibu-tuone.

Au unaumwa, anayekufanyia dialysis ni miaka 27. Usiposhuka utashangaa wewe unaendelea kuumwa na wenzako wanapona.

Katika somo la pili, Paulo anaeleza kwa kirefu juu ya upendo. Naomba mimi niongee juu ya tabia mbili za upendo zilizotajwa na Paulo: Upendo ni lazima uvumilie: Bila kuvumilia, huwezi kumpenda yeyote. Kuna watu wanaudhi, unawapenda lakini hawapendeki, unawatendea hiki hawaelewi-ni kama baadhi ya watoto wetu unakuta unasomesha kwa nguvu lakini hawatambui, wanakuona mbaya. Bila uvumilivu hutaweza kusomesha hata mtoto wako.

Hata baadhi ya wanandoa-unampenda mwenzako lakini yeye haelewi. Bila uvumilivu hakuna upendo.

Upendo pia wahusu kutokutangaza dhambi za wenzetu-upendo sio kutangaza sifa zako juu ya wengine, wewe uonekane kuwa mwema. Yahusu kumwona mwenzako kama nafsi yako pia.

©️Pd. Prosper Kessy OFMCap.

Maoni


Ingia utoe maoni