Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 4 ya Majilio (Jumapili, Desemba 19, 2021)  

Somo la 1

Mik. 5:2-4

Bwana asema: wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele. Kwa sababu hiyo atawatoa, hata wakati wa kuzaa kwake aliye na utungu; ndipo hayo mabaki ya nduguze watawarudia wana wa Israeli. Naye atasimama, na kulisha kundi lake kwa nguvu za Bwana, kwa enzi ya jina la Bwana, Mungu wake; nao watakaa; maana sasa atakuwa mkuu hata miisho ya dunia.

Wimbo wa Katikati

Zab. 80:1-2, 14-15, 17-18

Wewe uchungaye Israeli usikie,
Wewe uketiye juu ya makerubi, utoe nuru.
Uziamshe nguvu zako.
Uje, utuokoe.
(K) Ee Mungu, uturudishe, uangazishe uso wako nasi tutaokoka.

Ee Mungu wa majeshi, tunakusihi, urudi,
Utazame toka juu uone, uujilie mzabibu huu.
Na mche ule ulioupanda,
Kwa mkono wako wa kuume;
Na tawi lile ulilolifanya,
Kuwa imara kwa nafsi yako.
(K) Ee Mungu, uturudishe, uangazishe uso wako nasi tutaokoka.

Mkono wako na uwe juu yake,
Mtu wa mkono wa kuume;
Juu ya mwanadamu uliyemfanya,
Kuwa imara kwa nafsi yako;
Basi hatutakuacha kwa kurudi nyuma;
Utuhuishe nasi tutaliitia jina lako.
(K) Ee Mungu, uturudishe, uangazishe uso wako nasi tutaokoka.

Somo la 2

Ebr. 10:5-10

Ndugu zangu: Kwa hiyo ajapo ulimwenguni, Kristo asema, Dhabihu na toleo hukutaka, lakini mwili uliniwekea tayari; Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo; Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa) Niyafanye mapenzi yako, Mungu. Hapo juu asemapo, Dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzikataa, wala hukupendezwa nazo (zitolewazo kama ilivyoamuru torati), ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili. Katika mapenzi hayo tumepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.

Shangilio

Lk. 1:28

Aleluya, aleluya!
Mariamu akasema, tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.
Aleluya.

Injili

Lk. 1:39-45

Mariamu aliondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda, akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elisabeti. Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi? Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu. Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana.

Maoni


Ingia utoe maoni