Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Disemba 19, 2021

TAFAKARI DOMINIKA YA 4 YA MAJILIO MWAKA C

Funguka, jiandae kuzipokea baraka za Mwenyezi Mungu.

Wimbo wetu wa mwanzo unaotuongoza leo ni “dondokeni enyi mbingu toka juu na mawingu yamwage mwenye haki.” Yanatoka Isaya 45:8. Ni unabii uliotolewa na Isaya wakati wana wa Israeli wakiwa utumwani Babuloni. Kitendo cha wao kuwa utumwani kiliashiria ukosefu wa haki, kwamba dunia haina haki, wapo wengine wa kutawala na wengine kufanywa watumwa. Sasa anasema kwamba kutatokea mwenye haki, atakayetuletea haki. Atakayeweka mambo yote sawa. Lakini huyu walitamani atoke mbinguni, amwagwe kama mawingu toka juu kwani ndani ya hii dunia waliona hawezi kutokea huko mwenye haki kabisa kwani wote wanatunyanyasa. Tunataka atoke juu. Sasa, mbingu zitafunguka na atatumwa. Huyu ndiye mkombozi wetu.

Katika somo la kwanza, nabii Mika anaelezea tabia za huyu mfalme. Yeye kwa kipindi chake kutakuwa na amani na haki. Ataongoza kwa nguvu ya mkono wa Mungu na kipindi chake watu watakuwa salama. Haya yote yametimia kwa ujio wa Yesu. Yesu ndiye aliyehakikisha kwamba watu wake wanabakia salama. Alijitoa ili wengine wafaidi. Alikubali hata kufa msalabani lengo ni sisi tupone ndugu zangu.

Kwenye haya masomo yetu twajifunza mambo makuu mawili. Kwanza- Haya yalikuwa ni maneno matakatifu, ya Yehova anayeamuru baraka ziwamwagikie watu wake. Anawaeleza watu wake wazipokee na kutembea kati yao. Nchi inaambiwa sasa ifunguke, ijiandae kupokea baraka hizi. Baraka hizi inategemea jinsi nchi itakavyojifunua. Ikikataa kujifunua, itajifungia baraka hizi. Hii ni kweli.

Kristo alipokuja, alitegemea wale walijifunua kumpokea. Hawa walipewa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu. Sisi tushirikiane naye hasa pia kwenye sakramenti zetu. Tukishindwa kujiandaaa kupokea sakramenti hizo hakika hatutapa neema yoyote. Fungua moyo wako upate kuona baraka za Noeli, hizi tunazoimba kila mwaka. Ni kwa yule afunguae moyo tu ndiye anayeweza kuzielewa.

Cha pili ndugu zangu ni kwamba nasi tunahitaji watu wa namna hii mwenye tabia kama za mfalme huyu atakaye mwagwa toka mbinguni. Watu watakaojitolea ili sisi tubakie salama. Ewe mzazi lazima uhakikishe ukiwapo watoto wako, mke wako anabakia salama. Usifurahie unyanyasike, au watoto wako wanyanyasike, wauze uze vitu visivyofaa huko, au mke wako afanye biashara ajabu ajabu huko, atukanwe na kila mtu. Pambana. Hakikisha wale uliokabidhiwa wanabakia salama. Yesu alipokuwa na wanafuzi wake, walikuwa salama na hakuna aliyewagusa. Alikuwa tayari kuwatetea; nawe ufanye hivyohivyo.
Wengi kati ya wazazi wameshindwa kuwalinda watoto wao au wake zao. Tuwe vingozi wa namna hii.

Kina baba unakuta wanaamka nyumbani hawajui nini kitakachopikwa. Wameachia kila kitu chini ya mke wake, ama kweli hapa tunakosea sana, ni lazima tubadilike, ni uvivu, ni dhambi kama tutaendekeza jambo la namna hii.

Kiongozi huyu atafanikiwa kwa sababu ataongoza kwa nguvu ya Mungu. Sisi lazima tuongoze kwa nguvu ya Mungu. Tunahitaji viongozi wa namna hii. Ukikosa viongozi wasiomcha Mungu ni sababu ya wengi kuanguka. Hii ni kwa sababu binadamu ni viumbe tofauti, sio kama kuku unaoweza kuwafungia sehemu moja, hapana, ni kiumbe cha pekee. Wanambinu nyingi mno, unaweza kumshinda mwanadamu wa sasa kwa mbinu hii lakini jua kwamba sio wakati wote. Yaani mwanadamu ni 'complicated'. Halafu anatabia ya kudai haki, ukimtesa lazima itafikia mahali atakuja kudai haki yake tu. Hata kama ni mtumwa. Unaweza kumdanganya kwa muda tu lakini kwa wakati wote sio. Sisi tumweke Bwana mbele na hakika hatutakuwa sababu ya wengi kuanguka. Hii ni kwa sababu atakuwa na Bwana na hakika atafaulu katika mengi. Nasi tutambue kwamba tunashindwa kwa mengi kwa sababu ya kumuweka Bwana pembeni. Sisi tumweke Bwana karibu.

Katika somo la injili, tunakutana na Maria akienda kumtembelea Elisabethi. Safari hii inakuwa sababu ya furaha kwa yule Elisabeth na Yohane mbatizajil aliyekuwa tumboni mwa Elisabethi. Maria aliweza kuleta furaha hii kwa sababu ndani yake alikuwa na Yesu. Sisi tukazanie kuwa na Yesu ndani yetu, ndipo tutakapoweza kupeleka furaha mbele ya watu.
Ni kwa njia ya sala tu ndipo tutakapoweza kupeleka maneno ya matumaini mbele ya watu. Ukiwa na Bwana utaweza kumfurahisha yeyote anayekusikiliza. Hutapeleka moto kwa mwanzako au anayekuzunguka. Hakika atapelekewa habari njema kabisa.

Sisi tujiangalie, tumeshindwa kuwa mwanga kwa watu kwa sababu ya kupeleka moto, hasira, fujo kwa watu. Ukimtegemea Mungu hakika utaonyeshwa mazingira, namna ya kuongea, yote hayo yatakutokea.
Ukitaka kwenda kumshauri hata mwenzako kweli lazima ukae chini, uombe msaada toka kwa Mungu ili basi Bwana aingie ndani yako uweze kumshauri mwenzako huyo. Mara nyingi unakuta tunashindwa hata kusuluhisha kesi za wenzetu kwa sababu unakuta hatujasali, huna Bwana ndani. Unaishia kupeleka umbea. Sasa kweli utamsuluhisha yeyote? Na ndio maana hata vikesi vidogo vidogo vinatushinda kila wakati.

Umuhimu wa mama Maria; hapa unaonekana kabisa, ukisogea karibu yake ndivyo hivyo unavyokuwa karibu na Yesu na hakika utaweza kufurahi kama Elisabethi. Sisi hatuwezi kumfikia Yesu bila kuanzia kwa mama. Ndiyo imani yetu katoliki.

Tukimtanguliza mama, hakika tunamkaribia Yesu kwa haraka sana. Sisi tusiache kuwa karibu na mama kila wakati.

Zaburi ya wimbo wa katikati inatoka zaburi ya 80. Zaburi hii iliimbwa na wana wa Israeli kipindi walipokuwa wananyanyaswa na taifa la Asyria lililotaka kuwaangamiza kabisa. Sasa wanatamani ukombozi, wanamueleza Mungu jamani, njoo fanya kitu, usikubali tuteketekee kabisa. Wewe njoo Bwana.

Zaburi hii inatumika kuelezea umuhimu wa ukombozi wetu. Hata nasi tupo katika matamanio makubwa hivyo kwani Yesu ni wa muhimu sana kwetu na ni lazima tumpatie nafasi ya pekee.

©️Pd. Prosper Kessy OFMCap.

Maoni


Ingia utoe maoni