Jumanne. 26 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 32 ya Mwaka (Jumapili, Novemba 07, 2021)  

Somo la 1

1Fal 17:10-16

Eliya aliondoka, akaenda Sarepta; hata alipofika langoni pa mji, kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita, akamwambia, Niletee, nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa. Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, Niletee, nakuomba, kipande cha mkate mkononi mwako. Naye akasema, Kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe. Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao. Kwa kuwa Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi. Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi. Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa kinywa cha Eliya.

Wimbo wa Katikati

Zab 146:6-10

Bwana huishika kweli milele,
Huwafanyia hukumu walioonewa.
Huwapa wenye njaa chakula;
Naye huwafungua waliofungwa.
(K) Ee nafsi yangu, umsifu Bwana.

Bwana huwafumbua macho waliopofuka,
Naye huwainua walioinama.
Bwana huwapenda wenye haki,
Naam, huwahifadhi wageni.
(K) Ee nafsi yangu, umsifu Bwana.

Bwana huwategemeza yatima na mjane,
Bali njia ya wasio haki huipotosha.
Bwana atamiliki milele milele,
Mungu wako, ee Sayuni, kizazi hata kizazi.
(K) Ee nafsi yangu, umsifu Bwana.

Somo la 2

Ebr 9:24-28

Kristu hakuingia katika patakatifu palipofanyika kwa mikono, ndio mfano wa patakatifu halisi; bali aliingia mbinguni hasa, aonekane sasa usoni pa Mungu kwa ajili yetu; wala si kwamba ajitoe mara nyingi, kama vile kuhani mkuu aingiavyo katika patakatifu kila mwaka kwa damu isiyo yake; kama ni hivyo, ingalimpasa kuteswa mara nyingi tangu kuwekwa msingi wa ulimwengu; lakini sasa, mara moja tu, katika utimilifu wa nyakati, amefunuliwa, azitangue dhambi kwa dhabihu ya nafsi yake. Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu; kadhalika Kristo naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi; atatokea mara ya pili, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu.

Shangilio

Yn 14:6

Aleluya, aleluya!
Mimi ndimi njia, na ukweli, na uzima, asema Bwana; Mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Aleluya.

Injili

Mk 12:38-44

Yesu aliwaambia katika mafundisho yake, Jihadharini na waandishi, wapendao kutembea wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa masokoni, na kuketi mbele katika masinagogi, na viti vya mbele katika karamu; ambao hula nyumba za wajane, na kwa unafiki husali sala ndefu; hawa watapata hukumu iliyo kubwa. Naye akaketi kuielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi. Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa. Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina; maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia.

Maoni

Berno Mwendapole

Tumsifu Yesu Kristu, Hakika Mungu ni mwema kila wakati. Nashukuru sn kwa neno, Mungu awajalie na aendelee kuwatunza.

Kennedy Maundu

Tumsifu yesu kristu ....naomba sala ya maungamo

Ingia utoe maoni