Jumapili, Novemba 07, 2021
TAFAKARI YA DOMINIKA YA 32 YA MWAKA B
Karibuni ndugu zangu kwa misa takatifu Dominika ya leo. Leo tafakari yetu inaongozwa na wimbo wetu wa katikati unaotukaribisha tumsifu Mungu kwa sababu kila mmoja wetu amepewa kitu na yeye. Hujanyimwa kila kitu. Na katika magumu yoyote-lazima amekutafutia namna ya kutoka tu. Tunasikia zaburi hii ikisema kwamba ndiye yeye ampaye haki aliyeonewa, humpatia yatima na mjane haki yake na kuwalisha wenye njaa chakula. Ndiye yeye. Na kwa kila mwanadamu ametoa uwezo ambao kama atautumia, hakika haya hayatamshinda. Hakika ataufurahia huu ulinzi wa Bwana.
Katika somo la kwanza tunakutana na mama mmoja ndugu zangu mjane na maskini. Huyu mama kweli alikuwa katika shida na ulikuwa ndio mwisho wake. Yeye huitwa mjane wa Zarepta. Shida zilikuwa zimemshinda kabisa, zikatawala ufahamu wake, uhai wake, imani yake na maarifa yake. Anakutwa akiokota kuni za kuandaa chakula chake cha mwisho ili ale na kufa; yeye na mtoto wake. Kweli ni maneno ya kusikitisha.
Lakini anakutana na Elia, nabii anamletea maneno ya kumtia moyo, anamwambia achague njia nyingine, wazo ambalo ama kweli liliyapindua yale mawazo mabaya aliyokuwa nayo; njia iliyomfanya asikubali kushindwa na zile shida-bali imani yake iwe kubwa kuliko zile shida na kwa kufanya hivi anayaokoa maisha yake, maisha yake na mtoto na ya nabii huyu.
Kilichomuokoa huyu mama ni fundisho la Elia na imani ya Elia. Elia anamuonyesha kwamba Mungu ni juu ya hizo shida zako. Usikubali imani yako itawaliwe na shida. Hiki ni chanzo cha wewe kuanguka.
Katika somo la injili tunakutana na mama ambaye hakukubali imani yake itawaliwe na shida au hali aliyokuwa nayo. Yeye ndani ya udogo wake anaona kwamba bado ana cha kumpatia Mungu, hakubali shida zimshinde. Kwa kweli ana imani kuliko yule wa somo la kwanza na imani hii ndio inayomfanya akubalike machoni kwa Yesu na hakika huyu mama alikwenda mbinguni.
Ndugu zangu, masomo haya yanatufaa hasa sisi tulio na uwezo mdogo kifedha. Kuna mahali inafika tunatawaliwa na shida zetu, tunakosa imani kabisa, shida zinatufanya tunafanya mambo ya kijinga, tunashindwa hata kusali. Shida pia zinatufundisha tutafute visingizio hata kanisani hatutoi sadaka ati tukisema kwamba shida zetu zinatupatia "excemptions". Hapana! Hakuna kitu kama hiki. Hapa tunapotoka. Katika udogo wetu bado tunakitu cha kuweza kumtolea mwenyezi Mungu.
Au mtu unasema ati mimi ni mgonjwa siwezi kufanya kitu, acha tu nilale, Mungu ataniona-hapana-usikubali hali yako ikutawale, usitawaliwe na ugonjwa ukose hata imani au utende hata dhambi.
Ugonjwa usitawale imani yako bali imani yako iutawale.
Kweli tunahitaji watu wenye mitazamo kama ya huyu Elia. Wengi wetu tunawaridhisha watoto wetu mawazo kama ya huyu mama. Huyu mama anasema ati anasubiri kula leo na kesho afe; yeye na mtoto wake. Yaani huyu mama amekosa imani hata mtoto wake anaona atakufa tu. Mawazo kama ya huyu mama yanatukalia na wengi pia. Unakuta wazazi tunalia sisi ni mafukara bwana, na watoto wako wanaendeleza mawazo hayo wakisema; sasa mnataka muwe ombaomba wote?
Lazima ifikie wakati tuseme huu ni mwisho. Na kweli lazima kila mmoja awe kama Elia alete maneno ya kutia moyo ili watu wabadilike na sio watu wanaendelea kusema sisi ni maskini. Tutupe mbali mawazo kama haya. Ni kama unapita barabarani unakuta mtu mzima anamsukuma ombaomba ili apate kuomba-na yeye yupo nyuma anamsukuma. Yule anayemsukuma anakosa hekima. Inaonekana kwamba zile pesa wanakwendaga kugawana.
Kingine tutambue kwamba mawazo yetu finyu na uzembe wetu na uvivu unawafanya wengine wafe. Ogopa sana. Mtu ukishakabidhiwa majukumu ogopa uvivu ndugu yangu. Uvivu wako unataka uwaue? Kama ukiona huwezi jiuzulu, usituachie uvivu umalize watu. Ukipewa kitu endeleza, ukiwa mkurugenzi mahali endeleza hilo eneo. Usile tu, ule tu mwishowe unawaacha watu wafe kwashiakor. Achene hizo.
Wengine wanauza mali zote kwenye sehemu waliyoko. Na wewe dada unayekwenda kula pesa za watu-unaletewa tu unakula angalia-yatakutokea puani wewe dada. Badilika ndugu yangu.
Mama huyu japokuwa mwanzoni hali yake ya shida ilikuwa imeishinda imani yake, bado alikuwa na kaimani na alionyesha ukarimu kwa nabii na yeye akashiba na yeye akamuokoa na mtoto wake.
Na nyie jamani msiache kuwalisha manabii wenu. Wakiwaomba, wakisema wana njaa, labda akija akikuambia kwamba hana kiatu-ukarimu wako utakuokoa. Ukianza kuonyesha uchoyo kwa nabii ama kweli hutafanikiwa chochote. Kama huyu mama asingalifungua milango, angalikufa. Wengi wetu wamekufa na wamekosa baraka kwa sababu hawakufungua milango.
Wale mnaolalamika ati ni maskini leo iishe. Angalieni huyu mama. Na mtoe, achene kujitetea tetea. Na mchangie michango ya kanisa na zaka, inapaswa iwe hivyo. Kwa muda sasa mnasema sisi maskini-acheni-nyie ni matajiri jitume.
©️Pd. Prosper Kessy OFMCap.
Maoni
Ingia utoe maoni