Masomo ya Misa
Ijumaa ya 22 ya Mwaka (Ijumaa, Septemba 03, 2021)
Kol 1:15-20
Kristo Yesu ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake. Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye. Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote. Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae; na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake; kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni.
Zab 100:2-5
Mtumikieni Bwana kwa furaha;
Njoni mbele zake kwa kuimba;
(K) Njoni mbele ya Bwana kwa kuimba kwa furaha.
Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu;
Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake;
Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake.
(K) Njoni mbele ya Bwana kwa kuimba kwa furaha.
Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru;
Nyuani mwake kwa kusifu;
Mshukuruni, lihimidini jina lake;
(K) Njoni mbele ya Bwana kwa kuimba kwa furaha.
Kwa kuwa Bwana ndiye mwema;
Rehema zake ni za milele;
Na uaminifu wake vizazi na vizazi.
(K) Njoni mbele ya Bwana kwa kuimba kwa furaha.
Lk 5:33-39
Mafarisayo na waandishi walimwambia Yesu, Wanafunzi wa Yohana hufunga mara nyingi, na kuomba dua; na kadhalika wanafunzi wa Mafarisayo; lakini wanafunzi wako hula na kunywa! Lakini Yesu akawaambia, Je! Mwaweza kuwafanya wafunge walioalikwa arusini, akiwapo bwana arusi pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi, ndipo watakapofunga siku zile. Akawaambia na mithali, Hakuna akataye kiraka cha vazi jipya na kukitia katika vazi kuukuu; na kama akitia, amelikata lile jipya, na kile kiraka cha vazi jipya hakilingani na lile vazi kuukuu. Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu; na kama akitia, ile divai mpya itavipasua vile viriba, divai yenyewe itamwagika, na viriba vitaharibika. Lakini divai mpya sharti kutiwa katika viriba vipya. Wala hakuna anywaye divai ya kale akatamani divai mpya; kwa kuwa asema, Ile ya kale ndiyo iliyo njema.
Maoni
Ingia utoe maoni