Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Septemba 03, 2021

Ijumaa, Septemba 3, 2021
Juma la 22 la Mwaka


1Kor 4: 1-5;
Zab 36: 3-6, 27-28, 39-40;
Lk 5: 33-39


HAKUNA KIRAKA; HAKUNA KUCHANGANYA!

Karibuni sana ndugu zangu wapendwa kwa tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la kwanza toka katika waraka wa mtume Paulo kwa Wakolosai, Mtume Paulo anawaelezea Wakristo wa Kolosai juu ya ukuu wa Kristo. Anamtangaza Kristo kama sura ya Mfano wa Baba, Mzaliwa wa Kwanza wa viumbe vyote, amekuwako kabla ya viumbe vyote, na hakuna kilichopo bila Yeye.

Wakolosai ilibidi waelezewe juu ya ukuu huu kwani Wakolosai walishindwa kufaidi ukuu huu maishani mwao kwa sababu ya imani yao haba kwa Kristo. Wakristo wa Kolosai hawakuacha kuiabudu miungu yao, walizidi kuamini nguvu za mizimu, na wanamazingaumbwe na kushindwa kuiona nguvu ya Kristo ndani yao. Hivyo wakristo wa makanisa mengine walikuwa wanamfurahia Kristo na kuiona nguvu yake maishani mwao lakini Wakristo wa Kolosai walishindwa kwani hawakuukiri ukuu wa Kristo maishani mwao na kuishia kuteswa na shetani.

Somo hili linatoa ujumbe mkuu na kwetu pia.Wapo kati yetu tusioutambua ukuu wa Kristo bado. Wapo kati yetu ambao tunaogopa hata kulala chumbani wenyewe au ndani ya nyumba kwani tunaogopa ati tutapigwa na mapepo. Wapo kati yetu wenye hofu kali sana tena baadhi yetu ni watu wenye umri mkubwa. Tofauti yake unakutana na kijana au mtoto ambaye hana hofu, anatambua ukuu wa damu ya Yesu, anakuwa hodari hata kulala chumbani mwenyewe bila wasiwasi wowote, kwani hamwogopi shetani na hakika anatambua ukuu wa damu ya Kristo. Sisi tumsadiki Kristo, tusikubali kuteswa na shetani kiasi hiki. Tuirudie nguvu ya Kristo, tujifunze juu ya ukuu wa damu yake, tukubali itufunike. Tuone aibu kwa pale tunapopewa hofu na shetani au mizimu au roho chafu kiasi cha kushindwa hata kupata uhuru wa kufanya mambo yetu-Kristo ana nguvu kuliko roho hizi chafu.

Katika somo la Injili, Bwana Yesu anasisitiza kwamba divai mpya yafaa iwekwe kwenye viriba vipya. Viriba vipya ni mioyo mipya. Yesu yafaa aandaliwe moyo mpya na apokelewe ndani yake kama hakika tunataka kumfaidi. Lazima tuondoe viimani vyovyote vipotofu, tupende neno la Bwana na kuona nguvu yake ndani ya injili, hata masimulizi na hadithi zetu yafaa zibadilike, zihusiane na nguvu ya Kristo, na si masimulizi yahusuyo nguvu za mizimu, wachawi, namna zilivyo kuu. Picha tuangaliazo na hata vitabu tusomavyo na hata message tutumazo yafaa zieleze ukuu wa Kristo na nguvu ya damu yake. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni