Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Ijumaa ya 18 ya Mwaka (Ijumaa, Agosti 05, 2016)  

Somo la 1

Nah 1:15; 2:2; 3:1-3, 6-7

Tazama, juu ya milima iko miguu yake aletaye habari njema, atangazaye amani. Zishike sikukuu zako, Ee Yuda, uziondoe nadhiri zako; kwa maana yule asiyefaa kitu hatapita kati yako tena kamwe; amekwisha kukatiliwa mbali. Kwa maana Bwana anairudisha fahari ya Yakobo, kama fahari ya Israeli; maana watekao nyara wamewateka, na kuyaharibu matawi ya mizabibu yao. Ole wake mji wa damu! Umejaa mambo ya uongo na unyang'anyi; mateka hayaondoki. Kelele za mjeledi, kelele za magurudumu yafanyayo kishindo; na farasi wenye kupara-para, na magari ya vita yenye kuruka-ruka; mpanda farasi akipanda, na upanga ukimeta-meta, na mkuki ukimemetuka; na wingi wa waliouawa, na chungu kubwa ya mizoga; mizoga haina mwisho; wanajikwaa juu ya mizoga yao.Nami nitatupa uchafu uchukizao juu yako, kukufanya uwe mchafu, nami nitakufanya kuwa kitu cha kutazamwa kwa dharau. Hata itakuwa, wote wakutazamao watakukimbia, wakisema, Ninawi umeharibika; ni nani atakayeuhurumia? Nikutafutie wapi wafariji?

Wimbo wa Katikati

Kumb 32:35-36, 39, 41

Kisasi ni changu mimi, na kulipa, Wakati itakapoteleza miguu yao;
Maana siku ya msiba wao imekaribia, Na mambo yatakayowapata yatafanya haraka.
Kwa kuwa Bwana atawaamua watu wake, Atawahurumia watumwa wake,
(K) Naua mimi, nahuisha mimi

Fahamu sasa ya kuwa Mimi, naam, Mimi ndiye, Wala hapana Mungu mwingine ila Mimi;
Naua Mimi, nahuisha Mimi, Nimejeruhi, tena naponya; Wala hapana awezaye kuokoa katika mkono wangu,
(K) Naua mimi, nahuisha mimi

Nikiunoa upanga wangu wa umeme, Mkono wangu ukishika hukumu,
Nitawatoza kisasi adui zangu, Nitawalipa wanaonichukia.
(K) Naua mimi, nahuisha mimi

Shangilio

Mt 5:10

Aleluya, aleluya
Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.
Aleluya

Injili

Mt 16:24-28

Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona. Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? Kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake; ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. Amin, nawaambieni, Pana watu katika hawa wasimamao hapa, ambao hawataonja mauti kabisa, hata watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika ufalme wake.

Maoni


Ingia utoe maoni