Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumatano ya 18 ya Mwaka (Jumatano, Agosti 03, 2016)  

Somo la 1

Yer 31:1-7

Wakati huo, asema Bwana, nitakuwa Mungu wa jamaa zote za Israeli, nao watakuwa watu wangu. Bwana asema hivi, Watu wale walioachwa na upanga walipata neema jangwani; yaani, Israeli, hapo nilipokwenda kumstarehesha. Bwana alinitokea zamani, akisema, Naam nimekupenda kwa upendo wa milele, ndiyo maana nimekuvuta kwa fadhili zangu. Mara ya pili nitakujenga, nawe utajengwa, Ee bikira wa Israeli mara ya pili utapambwa kwa matari yako, nawe utatokea katika michezo yao wanaofurahi. Mara ya pili utapanda mizabibu juu ya milima ya Samaria; wapanzi watapanda, nao watayafurahia matunda yake. Maana kutakuwa siku moja, ambayo walinzi watalia juu ya vilima vya Efraimu, Inukeni, tukaende Sayuni, kwa Bwana, Mungu wetu. Maana Bwana asema hivi, Mwimbieni Yakobo kwa furaha, mkampigie kelele mkuu wa mataifa, tangazeni, sifuni, mkaseme, Ee Bwana, uwaokoe watu wako, mabaki ya Israeli.

Wimbo wa Katikati

Yer 31:10-13

Lisikieni neno la Bwana, enyi mataifa, litangazeni visiwani mbali; mkaseme,
Aliyemtawanya Israeli atamkusanya, na kumlinda, kama mchungaji alindavyo kundi lake.
(K) Bwana atatulinda kama mchungaji alindavyo kundi lake.

Kwa maana Bwana amemweka huru Yakobo, amemkomboa mkononi mwake aliyekuwa hodari kuliko yeye.
Nao watakuja, na kuimba katika mlima Sayuni, wataukimbilia wema wa Bwana
(K) Bwana atatulinda kama mchungaji alindavyo kundi lake.

Ndipo bikira atafurahi katika kucheza, na vijana na wazee pamoja;
maana nitageuza masikitiko yao kuwa furaha, nami nitawafariji, na kuwafurahisha waache huzuni zao.
(K) Bwana atatulinda kama mchungaji alindavyo kundi lake.

Shangilio

Lk 7:16

Aleluya, aleluya
Nabii mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia watu wake.
Aleluya

Injili

Mt 15:21-28

Wakati ule Yesu aliondoka huko, akaenda kando pande za Tiro na Sidoni. Na tazama, mwanamke Mkananayo wa mipaka ile akatokea, akampazia sauti akisema, Unirehemu, Bwana, Mwana wa Daudi; binti yangu amepagawa sana na pepo. Wala yeye hakumjibu neno. Nao wanafunzi wake wakamwendea, wakamwomba, wakisema, Mwache aende zake; kwa maana anapiga kelele nyuma yetu. Akajibu, akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Naye akaja akamsujudia, akisema Bwana, unisaidie. Akajibu, akasema, Si vema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa. Akasema, Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo yaangukayo mezani pa bwana zao. Ndipo Yesu akajibu, akamwambia, Mama, imani yako ni kubwa; na iwe kwako kama utakavyo. Akapona binti yake tangu saa ile.

Maoni


Ingia utoe maoni