Masomo ya Misa
Jumatatu ya 4 ya Mwaka (Jumatatu, Februari 01, 2021)
Ebr 11:32-40
Ndugu zangu niseme nini tena? Maana wakati usingenitosha kuleta habari za Gideoni na Baraka na Samsoni na Yeftha na Daudi na Samweli na za manabii; ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitenda haki, walipata ahadi, walifunga vinywa vya simba, walizima nguvu za moto, waliokoka na makali ya upanga. Walitiwa nguvu baada ya kuwa dhaifu, walikuwa hodari katika vita, walikimbiza majeshi ya wageni. Wanawake walipokea wafu wao waliofufuliwa. Lakini wengine waliumizwa vibaya hata kuuawa, wasikubali ukombozi, ili wapate ufufuo ulio bora; wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani; walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga; walizunguka-zunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya; (watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao), walikuwa wakizunguka-zunguka katika nyika na katika milima na katika mapango na katika mashimo ya nchi. Na watu hao wote wakiisha kushuhudiwa kwa sababu ya imani yao, hawakuipokea ahadi; kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea sisi kitu kilicho bora, ili wao wasikamilishwe pasipo sisi.
Zab 31:19-23
Jinsi zilivyo nyingi fadhili zako Ulizowawekea wakuchao;
Ulizowatendea wakukimbiliao Mbele ya wanadamu!
(K) Iweni hodari, mpige moyo konde, nyinyi nyote mnaongoja Bwana.
Utawasitiri na fitina za watu Katika sitara ya kuwapo kwako;
Utawaficha katika hema Na mashindano ya ndimi.
(K) Iweni hodari, mpige moyo konde, nyinyi nyote mnaongoja Bwana.
Bwana ahimidiwe;
kwa maana amenitendea Fadhili za ajabu katika mji wenye boma.
(K) Iweni hodari, mpige moyo konde, nyinyi nyote mnaongoja Bwana.
Nami nalisema kwa haraka yangu,
Nimekatiliwa mbali na macho yako;
Lakini ulisikia sauti ya dua yangu Wakati nilipokulilia.
(K) Iweni hodari, mpige moyo konde, nyinyi nyote mnaongoja Bwana.
Mpendeni Bwana, Ninyi nyote mlio watauwa wake.
Bwana huwahifadhi waaminifu,
Humlipa atendaye kiburi malipo tele.
(K) Iweni hodari, mpige moyo konde, nyinyi nyote mnaongoja Bwana.
Yn 15:15
Aleluya, aleluya,
Bwana anasema: Siwaiti tena watumwa, lakini ninyi nimewaita rafiki, kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.
Aleluya.
Mk 5:1-20
Yesu na wanafunzi wake walifika ng'ambo ya bahari mpaka nchi ya Wagerasi. Na alipokwisha kushuka chomboni, mara alikutana na mtu, ambaye ametoka makaburini, mwenye pepo mchafu; makao yake yalikuwa pale makaburini; wala hakuna mtu ye yote aliyeweza kumfunga tena, hata kwa minyororo; kwa sababu alikuwa amefungwa mara nyingi kwa pingu na minyororo, akaikata ile minyororo, na kuzivunja-vunja zile pingu; wala hakuna mtu aliyekuwa na nguvu za kumshinda. Na sikuzote, usiku na mchana, alikuwako makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikata-kata kwa mawe. Na alipomwona Yesu kwa mbali, alipiga mbio, akamsujudia; akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu usinitese. Kwa sababu amemwambia, Ewe pepo mchafu, mtoke mtu huyu. Akamwuliza, Jina lako nani? Akamjibu, Jina langu ni Legioni, kwa kuwa tu wengi. Akamsihi sana asiwapeleke nje ya nchi ile. Na hapo milimani palikuwa na kundi kubwa la nguruwe, wakilisha. Pepo wote wakamsihi, wakisema, Tupeleke katika nguruwe, tupate kuwaingia wao. Akawapa ruhusa. Wale pepo wachafu wakatoka, wakaingia katika wale nguruwe; nalo kundi lote likatelemka kwa kasi gengeni, wakaingia baharini, wapata elfu mbili; wakafa baharini. Wachungaji wao wakakimbia, wakaieneza habari mjini na mashambani. Watu wakatoka walione lililotokea. Wakamwendea Yesu, wakamwona yule mwenye pepo, ameketi, amevaa nguo, ana akili zake, naye ndiye aliyekuwa na lile jeshi; wakaogopa. Na wale waliokuwa wameona waliwaeleza ni mambo gani yaliyompata yule mwenye pepo, na habari za nguruwe. Wakaanza kumsihi aondoke mipakani mwao. Naye alipokuwa akipanda chomboni, yule aliyekuwa na pepo akamsihi kwamba awe pamoja naye; lakini hakumruhusu, bali alimwambia, Enenda zako nyumbani kwako, kwa watu wa kwenu, kawahubiri ni mambo gani makuu aliyokutendea Bwana, na jinsi alivyokurehemu. Akaenda zake, akaanza kuhubiri katika Dekapoli, ni mambo gani makuu Yesu aliyomtendea; watu wote wakastaajabu.
Maoni
Ingia utoe maoni