Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Februari 01, 2021

Jumatatu, Februari 1, 2021
Juma la 4 la Mwaka wa Kanisa

Ebr 11: 32-40;
Zab 31: 20-24;
Mk 5: 1-20.

KUBADILISHWA NA YESU!

Ndugu zangu karibu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Tuanze tafakari yetu kwa kuangalia zaburi ya wimbo wa katikati inayotualika tuwe hodari na kupiga moyo konde hasa sisi ambao tunamngoja Bwana. Zaburi hii inatuasa kwamba ulimwenguni kuna changamoto nyingi na wakati mwingine maisha yanatawaliwa na hali ya kukata tamaa. Hivyo tunaambiwa tuwe hodari, tusiwe legelege tunapaswa tuwe na imani.
Imani imewasaidia wengi kupigana hata na mambo yasiyowezekana, somo la kwanza linataja watu mbalimbali ambao maisha yao yalijaa imani wakafanikiwa kwa kila jambo. Walipata maadui wengi, walikutana hata na simba lakini kwasababu ya imani yao kwa Mungu walishinda.
Sisi nasi ndugu zangu tunateseka sana na kuyumbishwa na kila upepo wa ulimwengu kwasababu hatuna imani. Imani yetu imekuwa haba, tunatishiwa na vitu vidogo tunaogopa hata kumwacha Mungu. Tukiumwa kidogo tunazunguka kwa waganga mbali mbali, tunalishwa kila aina ya uchafu na masharti makali. Tujue wakutegemea ni Mungu, imani yetu ni muhimu sana, tuwe hodari.
Katika somo la Injili Yesu anamtoa pepo mchafu ambaye alikuwa akimtesa mtu kwa muda mrefu. Wengi walihangaika naye hata kumfunga lakini hawakuweza. Hili ni fundisho kwamba tunaweza pia kuhangaika na baadhi ya mambo au changamoto kwakutegemea watu lakini hatuwezi kufanikiwa kama Yesu hana nafasi.
Tumkaribishe Yesu, tuna matatizo mengi ambayo twaweza kuyafananisha na lile kundi la Pepo mchafu, ambayo yanatufunga na kututesa, tunahangika mnoo, na tumesahau kwamba Yesu ndiye msaada wetu. Twende kwake, tuwe hodari katika imani, sisi anatupenda kuliko viumbe vingine vyote, sisi ni wana wa Mungu ndio maana nguruwe wale hawakuwa muhimu kuliko mwanadamu. Yesu anatupenda sana tuwe na imani.

Maoni


Ingia utoe maoni