Masomo ya Misa
Ijumaa ya 15 ya Mwaka (Ijumaa, Julai 15, 2016)
Isa 38:1-6, 21-22, 7-8
Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, Bwana asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona. Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana, akasema, Ee Bwana, kumbuka haya, nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana. Ikawa, neno la Bwana likamjia Isaya, kusema, Enenda ukamwambie Hezekia, Bwana, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano. Nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu. Maana Isaya amesema, Na watwae mkate wa tini, wakauweke juu ya jipu, naye atapona. Tena Hezekia alikuwa amesema, Iko ishara gani ya kunionyesha ya kuwa nitapanda niingie nyumbani mwa Bwana?Jambo hili liwe ishara kwako, itokayo kwa Bwana, ya kuwa Bwana atalitimiza jambo hili alilolisema; Tazama, nitakirudisha nyuma kivuli madaraja kumi, ambayo kilishuka juu ya duara ya Ahazi kwa sababu ya jua. Basi jua likarudi madaraja kumi katika hiyo duara, ambayo limekwisha kushuka.
Zab 38:10-12, 16
Moyo wangu unapwita-pwita, Nguvu zangu zimeniacha;
Nuru ya macho yangu nayo imeniondoka.
(K) Umeniokoa na shimo la uharibifu, ee Bwana.
Wanipendao na rafiki zangu wanasimama mbali na pigo langu;
Naam, karibu zangu wamesimama mbali.
(K) Umeniokoa na shimo la uharibifu, ee Bwana.
Nao wanaoutafuta uhai wangu hutega mitego;
Nao wanaotaka kunidhuru hunena mabaya;
Na kufikiri hila mchana kutwa.
(K) Umeniokoa na shimo la uharibifu, ee Bwana.
Maana nalisema, Wasije wakanifurahia;
Mguu wangu ukiteleza wajitukuza juu yangu.
(K) Umeniokoa na shimo la uharibifu, ee Bwana.
Yn 10:27
Aleluya, aleluya
Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata.
Aleluya
Mt 12:1-8
Wakati ule Yesu alipita katika mashamba siku ya sabato; wanafunzi wake wakaona njaa, wakaanza kuvunja masuke, wakala. Na Mafarisayo walipoona, walimwambia, Tazama! Wanafunzi wako wanafanya neno ambalo si halali kulifanya siku ya sabato. Akawaambia, Hamkusoma alivyotenda Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wenziwe? jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaila mikate ile ya wonyesho, ambayo si halali kwake kuila wala kwa wale wenziwe, ila kwa makuhani peke yao? Wala hamkusoma katika torati, kwamba siku ya sabato makuhani hekaluni huinajisi sabato wasipate hatia? Lakini nawaambieni, kwamba hapa yupo aliye mkuu kuliko hekalu. Lakini kama mngalijua maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka, msingaliwalaumu wasio na hatia. Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato.
Maoni
Ingia utoe maoni