Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Kumbukumbu ya Kukatwa kichwa kwa Yohane Mbatizaji (Jumamosi, Agosti 29, 2020)  

Somo la 1

Yer 1:17-19

Neno la Bwana lilinijia, Haya basi, wewe jifunge viuno, ukaondoke, ukawaambie maneno yote niliyokuamuru; usifadhaike kwa ajili yao, nisije nikakufadhaisha wewe mbele yao. Maana, tazama, nimekufanya leo kuwa mji wenye boma, na nguzo ya chuma, na kuta za shaba, juu ya nchi yote; juu ya wafalem wa Yuda, na juu ya wakuu wake, na juu ya makuhani wake, na juu ya watu wa nchi hii. Nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, asema Bwana, ili nikuokoe.

Wimbo wa Katikati

Zab 71:1-6,15,17

Nimekukimbilia Wewe, Bwana,
Nisiaibike milele.
Kwa haki yako uniponye, uniopoe,
Unitegee sikio lako, uniokoe.
(K) Kinywa changu kitasimulia haki yako.

Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu,
Nitakakokwenda sikuzote.
Umeamuru niokolewe,
Ndiwe genge langu na ngome yangu.
Ee Mungu wangu, uniopoe mkononi mwa mkorofi.
(K) Kinywa changu kitasimulia haki yako.

Maana ndiwe taraja langu, Ee Bwana Mungu,
Tumaini langu tokea ujana wangu.
Nimekutegemea Wewe tangu kuzaliwa,
Ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu,
Ninakusifu Wewe daima.
(K) Kinywa changu kitasimulia haki yako.

Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako,
Mchana kutwa; maana sijui hesabu yake.
Ee Mungu, umenifundisha tokea ujana wangu,
Nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata milele.
(K) Kinywa changu kitasimulia haki yako.

Shangilio

Shangilio

Aleluya, aleluya,
Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki, maana ufalme wa mbinguni ni wao.
Aleluya.

Injili

Mk 6:17-29

Herode mwenyewe alikuwa ametuma watu, kumkamata Yohane, akamfunga gerezani, kwa ajili ya Herodia, mkewe Filipo ndugu yake; kwa kuwa amemwoa; kwa sababu Yohane alimwambia Herodi, Si halali kwako kuwa na mke wa nduguyo. Naye yule Herodia akawa akimvizia, akataka kumwua, asipate. Maana Herodi alimwogopa Yohane; akimjua kuwa ni mtu wa haki, mtakatifu, akamlinda; na alipokwisha kumsikiliza alifadhaika sana, naye alikuwa akimsikiliza kwa furaha. Hata ilipotokea siku ya kufaa, na Herode, sikukuu ya kuzaliwa kwake, alipowafanyia karamu wakubwa wake, na majemadari, na watu wenye cheo wa Galilaya; ndipo binti yake yule Herodia alipoingia, akacheza, akampendeza Herode na wale walioketi pamoja naye karamuni. Mfalame akamwambia yule kijana, Niombe lolote utakaloniomba nitakupa, hata nusu ya ufalme wangu. Basi akatoka, akamwuliza mamaye, Niombe nini? Naye akasema, Kichwa cha Yohane Mbatizaji. Mara akaingia kwa haraka mbele ya mfalme, akaomba akisema, Nataka unipe sasa hivi katika kombe kichwa cha Yohane Mbatizaji. Mfalme akafanya huzuni sana lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya hao walioketi karamuni, hakutaka kumkatalia. Mara mfalme akatuma askari, akaamuru kuleta kichwa chake. Basi, akaenda, akamkata kichwa mle gerezani, akakileta kichwa chake katika kombe, akampa yule kijana, naye yule kijana akampa mamaye. Wanafunzi wake waliposikia habari, walikwenda wakauchukua mwili wake, wakauzika kaburini.

Maoni


Ingia utoe maoni