Jumamosi, Agosti 29, 2020
Jumamosi, Agosti 29, 2020,
Juma la 21 la Mwaka
Kumbukumbu ya Kukatwa kichwa kwa Yohane Mbatizaji
Yer1: 2 17-19;
Zab 96:10-13
Mk 6:17-29
TUSIMAME KWA UKWELI!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tunaadhimisha sikuu ya kifo dini cha Yohane Mbatizaji. Yeye basi alimshuhudia Kristo tangu akiwa tumboni mwa Mama yake na hadi akatoa uhai wake akiutetea ukweli; ukweli ambao kiini chake ni Kristo.
Masomo yetu ya leo yanatutafakarisha zaidi kuhusu kifo dini chake na ushuhuda wake kama nabii. Somo la kwanza lahusu kuitwa kwa nabii Yeremia kama nabii. Yeye basi alitoka familia maskini, halafu aliitwa akiwa mdogo kabisa, na alijiona kutokuwa na uwezo. Lakini Mungu alimwambia kwamba yeye tayari amekwisha mchagua na kumpatia nguvu na uwezo wa kushindana na magumu yote. Na hivyo basi akamweleza kwamba asonge mbele hatashindwa.
Na kweli Yeremia alisonga mbele na kushinda. Alikutana na ugumu sana; kuna mahali ilifika akaona kwamba anashindwa kabisa na kifo ndio kinakaribia; alitishiwa na wana wa familia ya mfalme Zedekia wakimtaka atabiri kuendana na matakwa yao; lakini aligairi. Lakini cha ajabu aliweza kuvuka vigingi vyote hivyo; kweli Mungu alikuwa amemwahidia ulinzi na kweli aliuendeleza ulinzi huu.
Hapa ndugu zangu twajifunza kitu kikubwa sana. Kweli Mungu ametupatia nguvu za kuweza kushinda changamoto zote, Mungu hawezi kuleta changamoto ambayo hajakupatia nguvu za kuweza kutatua. Hata kama changamoto ni kubwa kiasi gani-jua kwamba tayari umekwishapewa nguvu za kuitatua-usiogope, tayari unao uwezo, Mungu kakupa nguvu. Wewe fanya, utafikiri kwamba unaanguka lakini hutaanguka kamwe. Hivyo tumtegemee Mungu. Tuache kukata tamaa, tusaidiane kwenye shida, Mungu tayari alikwishatupatia nguvu za kutosha, tusimwache kamwe.
Kwenye somo la injili tunakutana na namna mke wa mfalme Herode anavyoiongoza familia ya kifalme hadi idumbukie kwenye dhambi ya kumuua Yohane Mbatizaji. Huyu mama alitumia ushawishi wake wa kimama ndani ya familia kuiangusha familia kwenye kosa kubwa lililokuja kuwagharimu baadaye.
Somo hili latoa funzo nzito hasa kwa kina mama wa familia. Jueni kwamba mna ushawishi mkubwa ndani ya familia zenu. Msitumie huo ushawishi wenu vibaya kama Herodia. Namna hii mtaziletea familia maafa. Mama atambue mchango wake kwenye kujenga familia yake. kina mama tubakie pia zaidi kwenye ile tunu yetu ya kuwa watu wa huruma na wanaojali. Tusikubali hizi zitupotee kabisa, hizi ndizo tunu zinazomjenga mama; kina mama wengi siku hizi tunapenda kuiga maisha ya kibabe na matanuzi tukidhania kwamba hivi vitatuokoa-hili sio kweli. Tubakie kama tulivyo. Pale tulipokwisha kuwa kama kina Herodia jamani tuombe toba kwa Mungu.
Kifo cha Yohane Mbatizaji kitufanye tuwapende waume zetu Zaidi na majirani zetu na viongozi wetu wa dini-hasa wale wanaotuambia ukweli. Hawa ndio rafiki wa kweli. Lakini wale wanaotuacha tutende dhambi bila kutueleza hawa wanatupotosha kabisa.
Maoni
Ingia utoe maoni