Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Kumbukumbu ya Mt. Yohani Viane, Padre (Jumanne, Agosti 04, 2020)  

Somo la 1

Yer 30:1-2, 12-15, 18-22

Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, kusema, Bwana Mungu wa Israeli, asema hivi, ya kwamba, Uyaandike kitabuni maneno hayo yote niliyokuambia.Maana Bwana asema hivi, Maumivu yako hayaponyekani, na jeraha yako ni kubwa. Hapana mtu wa kukutetea; kwa jeraha yako huna dawa ziponyazo. Wote wakupendao wamekusahau; hawakutafuti; maana nimekujeruhi kwa jeraha ya adui, kwa adhabu ya mtu mkatili; kwa sababu ya ukubwa wa uovu wako, kwa sababu dhambi zako zilikuwa zimeongezeka. Mbona unalilia maumivu yako? Hayaponyeki maumivu yako; kwa sababu ya ukubwa wa uovu wako, kwa sababu dhambi zako zimeongezeka, nimekutenda haya. Bwana asema hivi, Tazama, nitarudisha tena hema za Yakobo zilizohamishwa, na kuyahurumia makao yake; nao mji huo utajengwa juu ya magofu yake wenyewe, nalo jumba litakaliwa, kama ilivyokuwa desturi yake. Tena kwao itasikiwa shukrani, na sauti yao wachangamkao; nami nitawazidisha, wala hawatakuwa wachache; tena nitawatukuza, wala hawatakuwa wanyonge. Watoto wao nao watakuwa kama zamani, na kusanyiko lao litathibitika mbele zangu, nami nitawaadhibu wote wawaoneao. Na mkuu wao atakuwa mtu wa kwao wenyewe, naye mwenye kuwatawala atakuwa mtu wa jamaa yao; nami nitamkaribisha, naye atanikaribia; maana ni nani aliye na moyo wa kuthubutu kunikaribia? Asema Bwana. Nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.

Wimbo wa Katikati

Zab 102:15-20, 28, 21-22

Kisha mataifa wataliogopa jina la Bwana,
Na wafalme wote wa dunia utukufu wako;
Bwana atakapokuwa ameijenga Sayuni,
Atakapoonekana katika utukufu wake,
Atakapoyaelekea maombi yake aliye mkiwa,
Asiyadharau maombi yao.
(K) Bwana atakapokuwa ameijenga Sayuni, atakapoonekana katika utukufu wake.

Kizazi kitakachokuja kitaandikiwa hayo,
Na watu watakaoumbwa watamsifu Bwana.
Maana ametazama toka patakatifu pake pa juu,
Toka mbinguni Bwana ameiangalia nchi,
Ili akusikie kuugua kwake aliyefungwa,
Na kuwafungua walioandikiwa kufa.
(K) Bwana atakapokuwa ameijenga Sayuni, atakapoonekana katika utukufu wake.

Wana wa watumishi wako watakaa,
Na wazao wao wataimarishwa mbele zako.
Watu walitangaze jina la Bwana katika Sayuni,
Na sifa zake katika Yerusalemu,
Pindi mataifa watapokusanyika pamoja,
Falme nazo ili kumtumikia Bwana.
(K) Bwana atakapokuwa ameijenga Sayuni, atakapoonekana katika utukufu wake.

Shangilio

Zab 119:135

Aleluya, aleluya,
Umwangazie mtumishi wako uso wako, na kunifundisha amri zako.
Aleluya.

Injili

Mt 15:1-2, 10-14

Ndipo Mafarisayo na waandishi toka Yerusalemu walipomwendea Yesu wakisema, Mbona wanafunzi wako huyahalifu mapokeo ya wazee, kwa maana hawanawi mikono walapo chakula. Akawaita makutano akawaambia Sikilizeni, mfahamu; Sicho kiingiacho kinywani kimtiacho mtu unajisi; bali kitokacho kinywani ndicho kimtiacho mtu unajisi. Ndipo wanafunzi wake walipomwendea, wakamwambia, Wajua ya kuwa Mafarisayo walipolisikia neno lile walichukizwa? Akajibu, akasema, Kila pando asilolipanda Baba yangu wa mbinguni litang'olewa. Waacheni; hao ni viongozi vipofu wa vipofu. Na kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, watatumbukia shimoni wote wawili.

Maoni


Ingia utoe maoni