Jumanne, Agosti 04, 2020
Jumanne, Agosti 4, 2020,
Juma la 18 la mwaka wa Kanisa
Yer 30:1-2, 12-15, 18-22;
Zab 101:16-23, 29;
Mt 14: 22-36.
KUFANYA YASIOWEZEKANA!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo basi neno la Bwana katika asubuhi hii linaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo Yuda inapewa unabii wa matumaini na Mwenyezi Mungu kupitia kinywa cha nabii Yeremia. Yeye basi anamwambia Yuda kwamba kwa kweli umepigwa sana na kwa sasa unajiona kana kwamba hutakaa uweze kupona tena. Majeraha yako yemezidi mno kiasi cha kujiona kwamba kwa kweli huponi tena. Lakini yeye anamhakikishia kwamba Bwana bado aweza yote, bado aweza kumgeuza na kumfanya tena awe mwana mpendwa wake, mwenye kupendwa na atakayefurahia tena maisha kama ilivyokuwa tena zamani. Anamwambia kwamba Mungu ni mwenye uwezo mwingi awezaye kubadili huzuni ikawa furaha na faraja kwenye maisha ya mkristo na mwanadamu yeyote.
Huu ni unabii wenye maneno ya matumaini sana kwetu ndugu zangu na leo basi tunaalikwa kumkimbilia Mungu katika unyonge wetu. Wengi wetu tupo katika vipigo vikali, tunakabiliana na hali ngumu ya maisha, watoto na vijana wetu ni wakaidi, waume zetu au wake zetu bado ni misalaba kwetu, masomo yetu bado yanatutesa sana shuleni na kuwa msalaba mzito sana kwetu, ugonjwa wetu umeshatupiga na kutuacha kwenye magumu mazito mno.
Lakini nabii Yeremia anatuambia leo kwamba Mungu ni mwenye uwezo wote, bado aweza kubadili magumu yetu haya na kutuletea kipindi cha matumaini tena, tukimtumainia atatugeuzia shida zetu hizi kuwa furaha tu. Basi ndugu zangu tuzidi kumkimbilia Mwenyezi Mungu; tukimwambia Bwana usitusahau, tupiganie, usituache, bado tuna matumaini makubwa sana kwako. Endelea kunisaidia Ee Yesu na Mwokozi wangu na kamwe usiniache. Kama uliweza kuwaletea wana wa Yuda kipindi cha faraja tena licha ya kwamba walikuwa wamedumbukia zaidi kwenye dhambi kubwa na nyingi, kwangu mimi waweza tena kuniletea kipindi kipya tena cha furaha Ee Mwenyezi Mungu, Mwokozi na Mkombozi wangu. Na kwa hiyo ninakuomba Ee Mwenyezi Mungu usiniache kamwe.
Injili yetu tunaona kwamba Yesu anakuwa chanzo cha matumaini kwa wanafunzi wake na kwa watu wa ile jamii waliyokuwa wakiiendea. Wanafunzi wake wanapatiwa matumaini baada ya kuogopa na kuingiwa na hofu kubwa wakimdhania Yesu kuwa ni mzimu baada ya kuhangaika na mawimbi mazito ndani ya bahari. Yesu anaingia tena katikati yao na kutuliza bahari na kuwaletea tena neema. Na kule anakokwenda anawaongezea wale watu wa yale maeneo matumaini Zaidi na Zaidi kwani watu wanaleta wagonjwa mbalimbali na kuponywa.
Nasi tuwe watu wa kuwaletea wengine matumaini. Tukifika mahali watu basi wafurahi na kutuletea wagonjwa, shida zao kama walivyofanya kwa Yesu. Ukifika eneo Fulani watu wafurahie na wapate ahueni kwa uwepo wako pale. Waswahili wanasema mgeni aje mwenyeji apone. Yesu aliwezea sana hili. Nasi tukitembelea mahali, tuwafanye watoto wa wajomba, mashangazi, wajukuu, mabinamu na wote wafurahi kwa ujio wetu. Hapa tunakuwa kama Yesu anavyokuwa kwa hawa watu wa kando ya ziwa la Genesareti.
Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni