Masomo ya Misa
Jumanne ya 10 ya Mwaka (Jumanne, Juni 09, 2020)
1Fal 17:7-16
Baada ya siku kupita, kile kijito kikakauka, kwa sababu mvua haikunya katika nchi. Neno la Bwana likamjia Eliya, kusema, Ondoka, uende Sarepta, ulio mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe. Basi, akaondoka, akaenda Sarepta; hata alipofika langoni pa mji, kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita, akamwambia, Niletee, nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa. Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, Niletee, nakuomba, kipande cha mkate mkononi mwako. Naye akasema, Kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; name ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe. Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanya kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kasha ujifanyie nafsi yako na mwanao. Kwa kuwa Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi. Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; nay eye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi. Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa kinywa cha Eliya.
Zab 4:2-5, 7-8;
Ee Mungu wa haki yangu, uniitikie niitapo;
Umenifanyizia nafasi wakati wa shida;
Unifadhili na kuisikia sala yangu.
Enyi wanadamu,
Hata lini utukufu wangu utafedheheka?
(K) Bwana, utuinulie nuru ya uso wako.
Bali jueni ya kuwa Bwana amejiteulia mtauwa;
Bwana atasikia nimwitapo.
Mwe na hofu wala msitende dhambi,
Tafakarini vitandani mwenu na kutulia.
(K) Bwana, utuinulie nuru ya uso wako.
Wengi husema, Nani atakayetuonyesha mema?
Bwana, utuinulie nuru ya uso wako.
Umenitia furaha moyoni mwangu,
Kupita yao wanapozidishiwa nafaka na divai.
(K) Bwana, utuinulie nuru ya uso wako.
Zab 27:11
Aleluya, aleluya.
Ee Bwana, unifundishe njia yako, na kuiongoza katika njia iliyonyoka.
Aleluya.
Mt 5:13-16
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu. Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.
Maoni
Ingia utoe maoni