Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Juni 09, 2020

Jumanne, Juni 9, 2020,
Juma la 10 la Mwaka wa Kanisa

1 Fal 17: 7-16;
Zab 4: 2-5, 7-8;
Mt 5: 13-16

CHUMVI NA MWANGA
Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana linaongozwa na zaburi yetu ya katikati kwa maneno yesemayo Ee Bwana utuangazie nuru ya uso wako na unisikilize nikuombapo. Haya ni maneno aliyoyasali Daudi akimuomba Mungu amngatue mikiononi mwa adui zake. Anamlilia Mungu amsaidie wakati aitapo.

Leo katika somo la kwanza tunamkuta sasa nabii Elia akimlilia Mungu na yeye ili amsaidie. Kwa neno la Bwana, Yeye alitabiri ujio ili utumike kuwaonya watu waache mabaya na kumrudia Mungu. Watu walishikwa na njaa sana lakini Mungu alimlisha kwa muujiza wa ajabu. Lakini leo kile kijito chake alichotegemea kupata maji ya kunywa nacho kinakauka na hivyo anabakia na njaa. Anamlilia Bwana naye Bwana anampeleka kwa mjane mmoja. Na kweli Elia alikuwa na njaa kali kwani kwa kitendo cha kumuona huyo mama tu akiokota kuni, alimwambia mara moja amletee kitu chakula. Mama huyu naye aliongea kitu cha ajabu. Alisema kabakiza kiasi kidogo sana cha unga kiasi kwamba ndiyo akisha kula, basi ataishia kufa. Elia katika njaa yake anamtia moyo yule mama amkandie tu ule unga na anamwambia kwamba hakika kiasi cha huu unga kitaongezeka. Na kweli haya yalitokea. Kweli huyu mama alikuwa na upendo mkubwa na imani kubwa na kutokana na ukarimu wake, anaepuka kifo bali wengine walikufa kwa njaa.

Hapa tuna la kujifunza. Kama Elia, tunaalikwa kumlilia Mungu. Hakika tusimuache. Yeye anazo namna nyingi za kutusaidia. Kweli shida tunazo na hivyo tumlilie Mungu na tufike kwake.

Kingine ni kwamba tumemsikia Elia alivyomwendea huyu mama na kumuomba amletee chakula. Kwa kweli Elia alikuwa ana njaa na ndio maana aliomba chakula kwanza. Ndivyo na sisi ndugu zangu. Akija mtu kwako akikuomba chakula kama huyu Elia, yaani kaamua kuja kwako tu kuomba, kamwe usikubali kumuacha mikono mitupu. Msaidie ndugu yangu. Kweli watu wanaokuja kuomba kwetu kama Elia alivyokuja ni wengi lakini wengi tunawafukuza.
Tumesikia jinsi yule mama alivyobarikiwa kwa kitendo chake hiki. Kweli alitenda hili kwa imani. Nasi ndugu zangu tujifunze kwa huyu. Wengi labda tungekuwa mbali sana. Labda tungetakiwa tuwe na uwezo mkubwa hata kifedha lakini kwa sababu tumewafukuza sana akina Elia wanaokuja kwetu kila siku, basi tumeishia kuwa hivi. Mimi kuna kitu kimoja ambacho labda naombeni mnisadie jamani.- yaani siku nikitoa pesa nikimpa mtu mwenye shida, siku hiyo nashangaa narudishiwa kama mara mbili na zaidi hivi. Kama nimetoa elfu tano, nashangaa naweza kupata hata elfu thelathini za ziada tu. Hili sidanganyi bali limekuwa likinitokea mara nyingi sana.

Katika injili yetu Yesu anatuambia kwamba sisi ni mwanga na chumvi ya ulimwengu. Kama chumvi ndugu zangu, tunapaswa kuyapatia maisha yetu ladha ili yawavutie wengine. Na kama chumvi, tunapaswa kuyatia maisha ya wengine ladha ili wayapende. Kuna baadhi ya watu wanajichukia wenyewe, wengine hawajiamini, wengine hawana matumaini. Kweli usimuache huyu bila kumpatia ladha.

Kingine kama mwanga, kweli lazima tuwe watu wa kutoa ushauri wa kufaa. Wengi wetu tunatoaga ushauri wa kushauri watu watende uovu. Watu wengi wameishia kutenda dhambi kama za uasherati kwa sababu huwa tunashauriana vibaya. Tunaenda na kuwaeleza wenzetu kwamba washiriki matendo haya hasa miongoni mwa vijana. Wasichana wadogo wamepata mimba kwa sababu ya kushauriwa vibaya. Wengine wameishia kula madawa ya kulevya au kwenye ulevi kwa sababu tunatoaga ushauri mbaya. Tunawaambia ati kushiriki matendo hayo ndio kuwa jembe au mjanja. Jamani, tuache kuwashauri watu vibaya. Tumsifu Yesu Kristo

Maoni


Ingia utoe maoni