Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumanne ya 7 ya Mwaka (Jumanne, Februari 25, 2020)  

Somo la 1

Yak 4:1-10

Vita vyatoka wapi, na mapigano yaliyoko kati yenu yatoka wapi? Si humu, katika tamaa zenu zifanyazo vita katika viungo vyenu? Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi!Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu. Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu. Au mwadhani ya kwamba maandiko yasema bure? Huyo Roho akaaye ndani yetu hututamani kiasi cha kuona wivu? Lakini hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema, Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu. Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili. Huzunikeni na kuomboleza na kulia. Kucheka kwenu na kugeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa hamu. Jidhilini mbele za Bwana, naye atawakuza.

Wimbo wa Katikati

Zab 55:5-10, 22

Nikasema, Ningekuwa na mbawa kama njiwa, Ningerukia mbali na kustarehe.
Ningekwenda zangu mbali, Ningetua jangwani.
(K)Umtwike Bwana mzigo wako naye atakutegemeza, hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele


Ningefanya haraka kuzikimbia Dhoruba na tufani.
Ee Bwana, uwaangamize, uzichafue ndimi zao,
(K)Umtwike Bwana mzigo wako naye atakutegemeza, hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele

Maana nimeona dhuluma na fitina katika mji.
Mchana na usiku huzunguka kutani mwake;
(K)Umtwike Bwana mzigo wako naye atakutegemeza, hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele

Umtwike Bwana mzigo wako naye atakutegemeza,
Hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele.
(K)Umtwike Bwana mzigo wako naye atakutegemeza, hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele

Shangilio

Gal 6:14

Aleluya, Aleluya
Nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu.
Aleluya

Injili

Mk 9:30-37

Yesu na wanafunzi wake walipita katikati ya Galilaya; naye hakutaka mtu kujua. Kwa sababu alikuwa akiwafundisha wanafunzi wake, akawaambia, Mwana wa Adamu yuaenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua; hata akiisha kuuawa, baada ya siku tatu atafufuka. Lakini hawakulifahamu neno lile, wakaogopa kumwuliza. Wakafika Kapernaumu; hata alipokuwamo nyumbani, akawauliza, Mlishindania nini njiani? Wakanyamaza; kwa maana njiani walikuwa wakibishana wao kwa wao, ni nani aliye mkubwa. Akaketi chini, akawaita wale Thenashara akawaambia, Mtu atakaye kuwa wa kwanza atakuwa wa mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote. Akatwaa kitoto, akamweka katikati yao, akamkumbatia, akawaambia, Mtu akimpokea mtoto mmoja wa namna hii kwa jina langu, anipokea mimi; na mtu akinipokea mimi, humpokea, si mimi, bali yeye aliyenituma.

Maoni


Ingia utoe maoni