Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Februari 25, 2020

Jumanne, Februari 25, 2020,
Juma la 7 la Mwaka wa Kanisa


Mk 9: 30-37.


HALI YA MAJUTO!

Katika somo la Injili tunawaona mitume wakibishana kuhusu nani mkubwa. Hali hii inafanana na tamaduni zetu, katika familia mbali mbali. Wakiwa njiani kuelekea Galilaya Yesu akiwa na Wanafunzi wake, Yesu alikuwa akifundisha. Badala ya kusikiliza, mitume walikuwa wakibishana wao kwa wao. Anawauliza wanaongea kuhusu nini?, na pale ukimya unatanda kwasababu mara moja dhamira zao ziliwashtaki. Walikuwa na mjadala ambao hauna maana, kwamba ni nani aliye mkubwa kati yao, na Yesu alivyowauliza mlikuwa mkibishana kuhusu nini waliona aibu kusema. Walitambua mjadala wao haukuwa na maana. Yesu anaendelea kuwapa mafundisho mazuri kuhusu unyenyekevu. Lakini leo sisi tutafakari juu ya somo tulilopata kwa hawa mitume, walivyosutwa na dhamiri zao baada ya Yesu kuwauliza swali.

Je, kusutwa na dhamiri ni nzuri? Je, inafurahisha kusutwa na dhamiri? Kwa huzuni kabisa katika ulimwengu wetu wa sasa, watu wengi wanakiuka maadili mema na amri za Mungu bila hata dhamiri zao kuwasuta. Lakini ukweli ni kwamba kusutwa na dhamiri ni kitu kizuri! Dhamiri kuuma ni wazi kwamba umetambua kosa lako! Dhamiri katika hali hii ni dhahiri kwamba ipo hai. Lakini katika nyakati zetu tatizo la kufa kidhamiri ni tatizo kubwa. Watu wanakosa lakini hawataki kukubali kwamba wamekakosea, hutumia kila njia kuonesha kwamba kosa sio lake. Dhamiri ikifa pia hufikia hali ya kuhalalisha dhambi na kuona ni kitu cha kawaida.

Somo tunalopata kutoka katika Injili hii ni kwamba, ni vizuri kuwa na dhamiri hai, ili tunapokosa tuweze kuhisi uchungu unao tuita kutubu. Ni vizuri kusikiliza dhamiri zetu zinavyotuita tubadilike na kuwa watu wema. Hili litatufanya daima tuwe wanyenyekevu na kuungama dhambi zetu.

Je, wewe una dhamiri hai inayokusaidia kurudi kwa Mungu unavyo jikuta ukipotea? Ruhusu hali hii ya fadhila ili Bwana wetu aweze kuwa kiongozi wako katika maisha ya kila siku.

Sala:
Bwana ninakukabidhi dhamiri yangu. Ninatambua kuwa dhamiri yangu ni hekalu, sehemu takatifu, sehemu nilioitwa kukutana nawe na kusikiliza sauti yako. Ninaomba dhamiri yangu ifunguke katika kupokea ukweli wa Injili yako ili niweze kuongozwa nawe kila siku. Yesu, nakuamini wewe.
Amina

Maoni


Ingia utoe maoni