Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 31 ya Mwaka (Jumapili, Novemba 03, 2019)  

Somo la 1

Hek 11:22-12:2

Ulimwengu wote mbele zako Bwana, ni kama chembe moja katika mizani na mfano wa tone moja la umande lishukalo asubuhi juu ya ardhi. Lakini Wewe unawahurumia watu wote, kwa sababu unao uweza wa kutenda mambo yote; nawe wawaachilia wanadamu dhambi zao, ili wapate kutubu. Kwa maana Wewe wavipenda vitu vyote vilivyopo, wala huchukii kitu chochote ulichokiumba.Kwa kuwa hulingalifanya kamwe kitu chochote kama ungalikichukia; tena kitu cho chote kingaliweza kudumu, ila kwa mapenzi yako? au kitu kisichoumbwa nawe kingaliwezaje kuhifadhika? Lakini Wewe unaviachilia vyote, kwa kuwa ni vyako, Ee Mfalme Mkuu, mpenda roho za watu, maana roho yako isiyoharibika imo katika vyote. Kwa hiyo wawathibitishia kidogo kidogo hatia yao, wale wanaokengeuka kutoka katika njia njema; wawaonya, ukiwakumbusha kwa mambo yale yale wanayokosa, ili waokoke katika ubaya wao, na kukuamini Wewe, Bwana.

Wimbo wa Katikati

Zab 145: 1-2, 8-11, 13-14

Ee Mungu wangu, Mfalme, nitakutukuza,
Nitalihimidi jina lako milele na milele.
Kila siku nitakuhimidi,
Nitalisifu jina lako milele na milele.
(K) Ee Mungu Mfalme wangu, Nitalitukuza jina lako milele

Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma,
Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema,
Bwana ni mwema kwa watu wote,
Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote.
(K) Ee Mungu Mfalme wangu, Nitalitukuza jina lako milele

Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru,
Na wacha Mungu wako watakuhimidi.
Wataunena utukufu wa ufalme wako,
Na kuuhadithia uweza wako.
(K) Ee Mungu Mfalme wangu, Nitalitukuza jina lako milele

Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote,
Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote.
Bwana huwategemeza wote waangukao,
Huwainua wote walioinama chini.
(K) Ee Mungu Mfalme wangu, Nitalitukuza jina lako milele

Somo la 2

2The 1:11-2:2

Kwa hiyo twawaombea ninyi sikuzote, ili Mungu wetu awahesabu kuwa mmekustahili kuitwa kwenu, akatimiza kila haja ya wema na kila kazi ya imani kwa nguvu; jina la Bwana wetu Yesu litukuzwe ndani yenu, nanyi ndani yake, kwa neema ya Mungu wetu na ya Bwana Yesu Kristo. Basi, ndugu, tunakusihini, kwa habari ya kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, na kukusanyika kwetu mbele zake, kwamba msifadhaishwe upesi hata kuiacha nia yenu, wala msisitushwe, kwa roho, wala kwa neno, wala kwa waraka unaodhaniwa kuwa ni wetu, kana kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwapo.

Shangilio

Lk 2:36

Aleluya, aleluya
Kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kusimama mbele za Mwana wa Adamu.
Aleluya

Injili

Lk 19:1-10

Yesu alipoingia Yeriko alipita katikati yake.Na tazama, palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni tajiri. Huyu alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani, asiweze kwa sababu ya umati wa watu, maana ni mfupi wa kimo. Akatangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kuipitia njia ile. Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako. Akafanya haraka, akashuka, akamkaribisha kwa furaha. Hata watu walipoona, walinung'unika wote, wakisema, Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi. Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne. Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu. Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.

Maoni


Ingia utoe maoni