Masomo ya Misa
Kumbukumbu ya Mtakatifu Karoli Boromeo (Askofu) (Jumatatu, Novemba 04, 2019)
Rum 11:29-36
Karama za Mungu hazina majuto, wala mwito wake. Kwa maana kama ninyi zamani mlivyomwasi Mungu, lakini sasa mmepata rehema kwa kuasi kwao; kadhalika na hao wameasi sasa, ili kwa kupata rehema kwenu wao nao wapate rehema. Maana Mungu amewafunga wote pamoja katika kuasi ili awarehemu wote. Jinsi zilivyo kuu utajiri na hekima na maarifa ya Mungu! Hukumu zake hazichunguziki, wala njia zake hazitafutikani! Maana ni nani aliyeijua nia ya Bwana? Au ni nani aliyekuwa mshauri wake? Au ni nani aliyempa yeye kitu kwanza, naye atalipwa tena? Kwa kuwa vitu vyote vyatoka kwake, viko kwa uweza wake, tena vinarejea kwake. Utukufu una yeye milele. Amina.
Zab 69:29-30, 32-33, 35-36
Nami niliye maskini na mtu wa huzuni,
Mungu, wokovu wako utaniinua.
Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo,
Nami nitamtukuza kwa shukrani.
(K) Kwa wingi wa fadhili zako unijibu Ee Mungu.
Walioonewa watakapoona watafurahi;
Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe.
Kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji,
Wala hawadharau wafungwa wake.
(K) Kwa wingi wa fadhili zako unijibu Ee Mungu.
Maana Mungu ataiokoa Sayuni, na kuijenga miji ya Yuda,
Na watu watakaa ndani yake na kuimiliki.
Wazao wa watumishi wake watairithi,
Nao walipendao jina lake watakaa humo.
(K) Kwa wingi wa fadhili zako unijibu Ee Mungu.
Lk 14:12-14
Yesu alimwambia na yule aliyemwalika, Ufanyapo chakula cha mchana au cha jioni, usiwaite rafiki zako, wala ndugu zako, wala jamaa zako, wala jirani zako wenye mali; wao wasije wakakualika wewe ukapata malipo. Bali ufanyapo karamu waite maskini, vilema, viwete, vipofu, nawe utakuwa heri, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa; kwa maana utalipwa katika ufufuo wa wenye haki.
Maoni
Ingia utoe maoni