Masomo ya Misa
Jumatano ya 22 ya Mwaka (Jumatano, Septemba 04, 2019)
Kol 1:1-8
Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo, ndugu yetu, kwa ndugu watakatifu, waaminifu katika Kristo, walioko Kolosai. Neema na iwe kwenu, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu. Twamshukuru Mungu, Baba yake Bwana wetu Yesu Kristo, siku zote tukiwaombea; tangu tuliposikia habari za imani yenu katika Kristo Yesu, na upendo mlio nao kwa watakatifu wote; kwa sababu ya tumaini mlilowekewa akiba mbinguni; ambalo habari zake mlizisikia zamani kwa neno la kweli ya Injili; iliyofika kwenu, kama ilivyo katika ulimwengu wote, na kuzaa matunda na kukua, kama inavyokua kwenu pia, tangu siku mlipoisikia mkaifahamu sana neema ya Mungu katika kweli; kama mlivyofundishwa na Epafra, mjoli wetu mpenzi, aliye mhudumu mwaminifu wa Kristo kwa ajili yenu; naye alitueleza upendo wenu katika Roho.
Zab 52:8-9
Bali mimi ni kama mzeituni Umeao katika nyumba ya Mungu.
Nazitumainia fadhili za Mungu milele na milele.
(K) Nazitumainia fadhili za Mungu milele na milele.
Nitakushukuru milele kwa maana umetenda;
Nitalingojea jina lako kwa kuwa ni jema;
Mbele ya wacha Mungu wako.
(K) Nazitumainia fadhili za Mungu milele na milele.
Lk 4:38-44
Yesu alitoka katika sinagogi, akaingia katika nyumba ya Simoni. Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa ameshikwa na homa kali, wakamwomba kwa ajili yake. Akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, ikamwacha; mara hiyo akaondoka, akawatumikia. Na jua lilipokuwa likichwa, wote waliokuwa na wagonjwa wenye maradhi mbali mbali waliwaleta kwake, akaweka mikono yake juu ya kila mmoja akawaponya. Pepo nao waliwatoka watu wengi, wakipiga kelele na kusema, Wewe u Mwana wa Mungu. Akawakemea, asiwaache kunena, kwa sababu walimjua kuwa ndiye Kristo. Hata kulipokucha alitoka akaenda mahali pasipokuwa na watu; makutano wakawa wakimtafuta-tafuta, wakafika kwake, wakataka kumzuia asiondoke kwao. Akawaambia, Imenipasa kuihubiri habari njema ya ufalme wa Mungu katika miji mingine pia; maana kwa sababu hiyo nalitumwa. Basi, alikuwa akihubiri katika masinagogi ya Galilaya.
Maoni
Ingia utoe maoni