Jumanne. 26 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Septemba 04, 2019

Jumatano, Septemba 4, 2019,
Juma la 22 la Mwaka

Sala ya Kanisa (Zaburi)-Juma la 2
______
MASOMO YA MISA
Kol 1: 1-8;
Zab 52: 10-11;
Lk 4: 38-44
_________

KUWA NA YESU DAIMA!

Katika Injili ya leo, tunaona Yesu akimponya mkwewe Simoni. Mara nyingi Yesu aliponya kwa kugusa, lakini leo ana amuru kwa neno la mamlaka na kuponya kwa kuamuru. Msisitizo unaoneshwa kwenye Injili, ugonjwa ndio unao amuriwa, kama Yesu alivyo amuru mawimbi ya bahari ya Galilaya kwa mamlaka, “hali ikawa shwari” na Amani ikawapo (Mk 4: 39), na mawimbi yakatulia. Watu walitambua mamlaka yake, hata pepo aliyemtoka mtu alisema ‘tunakufahamu wewe u Mwana wa Mungu.’

Siku iliyo fuata Yesu alienda mahali peke yake kusali, kuwa mbele ya Baba yake wa mbinguni. Ingawaje Yesu alikuwa ametumia muda wote wa jioni ya jana yake kwa ajili ya watu, lakini watu walitaka kuwa naye zaidi. Alikuwa ametoka kidogo kwenda kusali lakini watu walikuwa wakimtafuta na kuwa naye zaidi. Na walipo mpata walimuomba abaki nao zaidi. Yesu alionekana vizuri sana kwa watu hawa.

Sehemu hii inatuonesha hamu yetu pia ya kutaka kuwa na Yesu. Tunapaswa kutamani kubaki na Yesu daima. Tunapaswa tunapo enda kulala abaki katika akili zetu, tuamke kwa kumuomba na kumuomba abaki nasi siku nzima. Tunapaswa kuwa na mapendo hayo hayo kwa Yesu kama hawa watu walivyokuwa na mapendo kwa Yesu. Kuonesha mapendo hayo kwake ni hatua ya kwanza ya kumruhusu awe nasi kila siku na nyakati zote.

Jaribu kutafakari leo juu ya hamu yako ya kuwa na Yesu au ukosefu wako wa kutokutamani kuwa naye. Je, kuna wakati unatamani asiwe nawe? Au umeshawahi kuwa kama hawa watu waliokuwa na hamu ya kukaa tu na Bwana? Chagua kukaa na Yesu, upate Amani na salama ya maisha yote.

Sala:
Bwana, ninatamani uwe nami muda wote katika maisha yangu. Ninakuomba nikutafute wewe daima na niwe msikivu wa uwepo wako katika maisha yangu. Yesu, nakuamini wewe.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni