Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumatano ya 20 ya Mwaka (Jumatano, Agosti 21, 2019)  

Somo la 1

Amu 9:6-15

Watu wote wa Shekemu walikusanyika pamoja, na jamaa yote ya Milo, wakaenda na kumtawaza Abimeleki awe mfalme, karibu na huo mgandi ulio karibu na ngome iliyo katika Shekemu. Kisha walipomwambia huyo Yothamu, yeye akaenda, akasimama juu ya kilele cha kilima cha Gerizimu, akapaza sauti yake, akapiga kelele, na kuwaambia, Nisikieni mimi, enyi watu wa Shekemu, ili kwamba Mungu naye apate kuwasikia ninyi. Siku moja miti ilitoka ili kuutia mmoja mafuta uwe mfalme juu yao; ikauambia mti mzeituni, Tawala wewe juu yetu. Lakini huo mzeituni ukaiambia, Je! Niache mafuta yangu, ambayo kwangu mimi watu wamheshimu Mungu na wanadamu, ili niende nikayonge-yonge juu ya miti? Kisha miti ikauambia mtini, Njoo wewe, utawale juu yetu. Lakini huo mtini ukaiambia, Je! Niuache utamu wangu, na matunda yangu mazuri, niende nikayonge-yonge juu ya miti? Kisha miti ikauambia mzabibu, Njoo wewe, utawale juu yetu. Huo mzabibu nao ukaiambia, Je! Niiache divai yangu, ambayo humfurahisha Mungu na wanadamu, ili niende nikayonge-yonge juu ya miti? Ndipo hiyo miti yote ikauambia mti wa miiba, Njoo wewe, utawale juu yetu. Huo mti wa miiba ukaiambia miti, Kwamba ninyi mwanitia mafuta niwe mfalme juu yenu kwelikweli, basi njoni mtumaini kivuli changu; na kwamba sivyo, na utoke moto katika mti wa miiba na kuiteketeza mierezi ya Lebanoni.

Wimbo wa Katikati

Zab 21:1-6

Ee Bwana, mfalme atazifurahia nguvu zako,
Na wokovu wako ataufanyia shangwe nyingi sana.
Umempa haja ya moyo wake,
Wala hukumzuilia matakwa ya midomo yake.
(K) Ee Bwana, mfalme atazifurahia nguvu zako.

Maana umemsogezea baraka za heri,
Umemvika taji ya dhahabu safi kichwani pake.
Alikuomba uhai, ukampa,
Muda mrefu wa siku nyingi, milele na milele.
(K) Ee Bwana, mfalme atazifurahia nguvu zako.

Utukufu wake ni mkuu kwa wokovu wako,
Heshima na adhama waweka juu yake.
Maana umemfanya kuwa baraka za milele,
Wamfurahisha kwa furaha ya uso wako.
(K) Ee Bwana, mfalme atazifurahia nguvu zako.

Injili

Mt 20:1-16

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu mwenye nyumba aliyetoka alfajiri kwenda kuajiri wakulima awapeleke katika shamba lake la mizabibu. Naye alipokwisha kupatana na wakulima kuwapa kutwa dinari, aliwapeleka katika shamba lake la mizabibu. Akatoka mnamo saa tatu, akaona wengine wamesimama sokoni wasiokuwa na kazi; na hao nao akawaambia, Enendeni nanyi katika shamba langu la mizabibu, na iliyo haki nitawapa. Wakaenda. Akatoka tena mnamo saa sita na saa kenda, akafanya vile vile. Hata kama saa kumi na moja akatoka, akakuta wengine wamesimama, akawaambia, Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi? Wakamwambia, Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri. Akawaambia, enendeni nanyi katika shamba la mizabibu. Kulipokuchwa, yule bwana wa shamba akamwambia msimamizi wake, Waite wakulima, uwalipe ujira wao, ukianzia wa mwisho hata wa kwanza. Na walipokuja wale wa saa kumi na moja, walipokea kila mtu dinari. Na wale wa kwanza walipokuja, walidhani kwamba watapokea zaidi; na hao pia wakapokea kila mtu dinari. Basi wakiisha kuipokea, wakamnung'unikia mwenye nyumba, wakisema, Hao wa mwisho wametenda kazi saa moja tu, nawe umewasawazisha na sisi tuliostahimili taabu na hari za mchana kutwa. Naye akamjibu mmoja wao, akamwambia, Rafiki, sikudhulumu; hukupatana nami kwa dinari? Chukua iliyo yako, uende zako; napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe. Si halali yangu kutumia vilivyo vyangu kama nipendavyo? Au jicho lako limekuwa ovu kwa sababu ya mimi kuwa mwema? Vivyo hivyo wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho.

Maoni


Ingia utoe maoni