Masomo ya Misa
Jumatano ya 14 ya Mwaka (Jumatano, Julai 10, 2019)
Mwa 41 :55-57; 42 :5-7, 17-24
Nchi yote ya Misri ilipoona njaa, watu walilia Farao awape chakula. Farao akawaambia Wamisri wote, Enendeni kwa Yusufu; atakavyowaambia, fanyeni. Njaa ikawa katika dunia yote pia. Yusufu akazifungua ghala zote, akawauzia Wamisri. Njaa ikawa nzito katika nchi ya Misri. Watu wa nchi zote wakaja Misri kwa Yusufu; ili wanunue nafaka; kwa sababu njaa imekuwa nzito katika dunia yote. Wana wa Israeli wakaja wanunue chakula miongoni mwao waliokuja, kwa kuwa kulikuwa na njaa katika nchi ya Kanaani. Naye Yusufu alikuwa ni liwali juu ya nchi, ndiye aliyewauzia watu wote wa nchi. Nao ndugu zake Yusufu wakaja, wakainama kifudifudi mbele yake. Yusufu akawaona nduguze akawatambua, lakini alijifanya kama mgeni kwao. Akasema nao kwa maneno makali, akawaambia, Mmetoka wapi ninyi? Wakasema, Tumetoka nchi ya Kanaani, ili tununue chakula. Akawatia wote gerezani siku tatu. Yusufu akawaambia siku ya tatu, Fanyeni hivi, mkaishi, maana mimi namcha Mungu. Kama ni wa kweli ninyi, ndugu yenu mmoja na afungwe gerezani, nanyi nendeni mkachukue nafaka kwa njaa ya nyumba zenu, mkamlete ndugu yenu mdogo kwangu; hivyo maneno yenu yatahakikishwa, wala hamtakufa. Ndivyo walivyofanya. Wakaambiana, Kweli sisi tulimkosa ndugu yetu, kwa kuwa tuliona shida ya roho yake, alipotusihi, wala hatukusikia; kwa hiyo shida hii imetupata. Reubeni akajibu, akawaambia, Sikuwaambia, nikisema, msimkose kijana? Wala hamkusikia; kwa hiyo damu yake inatakwa tena. Wala hawakujua ya kwamba Yusufu anawasikia, kwa sababu alikuwapo mkalimani kati yao. Akajitenga nao akalia. Kisha akawarudia, na kusema nao, akamtwaa Simeoni miongoni mwao, akamfunga mbele ya macho yao.
Zab 33: 1-2, 10-11, 18-19
Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki,
kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.
Mshukuruni Bwana kwa kinubi,
Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa.
(K) Ee Bwana fadhili zako zikae nasi, kama vile tulivyokungoja Wewe.
Bwana huyabatilisha mashauri ya mataifa,
huyatangua makusudi ya watu.
Shauri la Bwana lasimama milele,
makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi.
(K) Ee Bwana fadhili zako zikae nasi, kama vile tulivyokungoja Wewe.
Tazama jicho la Bwana li kwa wamchao
Wazingojeao fadhili zake.
Yeye huwaponya nafsi zao na mauti
na kuwahuisha wakati wa njaa.
(K) Ee Bwana fadhili zako zikae nasi, kama vile tulivyokungoja Wewe.
Kol 3 : 16,17
Aleluya, Aleluya,
Neno la Kristo Tikae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkishukuru Mungu Baba kwa Yeye.
Aleluya.
Mt 10:1-7
Yesu aliwaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Na majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya; Wa kwanza Simoni aliyeitwa Petro, na Andrea nduguye; Yakobo wa Zebedayo, na Yohane nduguye; Filipo, na Bartholomayo; Tomaso, na Mathayo mtoza ushuru; Yakobo wa Alfayo, na Thadayo; Simoni Mkananayo, na Yuda Iskariote, naye ndiye mwenye kumsaliti. Hao Thenashara Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema. Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria msiingie. Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia.
Maoni
Ingia utoe maoni