Masomo ya Misa
Jumanne ya 14 ya Mwaka (Jumanne, Julai 09, 2019)
Mwa. 32:23-33
Yakobo aliondoka usiku ule akawatwaa wakeze wawili, na vijakazi wake wawili, na wanawe kumi na mmoja, akavuka kivuko cha Yaboki. Akawatwaa, akawavusha mto, akavusha na vyote alivyokuwa navyo. Yakobo akakaa peke yake; na mtu mmoja akashindana naye mweleka hata alfajiri. Naye alipoona ya kuwa hamshindi, alimgusu panapo uvungu wa paja lake; ukateguka uvungu wa paja la Yakobo alipokuwa akishindana naye. Akasema, Niache, niende, maana kunapambazuka. Akasema, Sikuachi, usiponibariki. Akamwuliza, Jina lako n’nani? Akasema, Yakobo. Akamwambia, Jina lako hutaitwa tena Yakobo, ila Israeli, maana umeshindana na Mungu, na watu, nawe umeshinda. Yakobo akamwuliza, akasema, Niambie, tafadhali, jina lako? Akasema, Kwa nini waniuliza jina langu? Akambariki huko. Yakobo akapaita mahali pale, Penueli, maana alisema, Nimeonana na Mungu uso kwa uso, na nafsi vangu imeokoka. Jua likamzukia akivuka Penueli, akachechemea kwa sababu ya paja la mguu wake. Kwa hiyo wana wa Israeli hawali ule mshipa ulio katika uvungu wa paja hata leo; maana alimgusa Yakobo panapo uvungu wa paja katika mshipa wa kiuno.
Zab 17:1-3, 6-8, 15
Ee Bwana, usikie haki, ukisikilize kilio changu,
Utege sikio lako kwa maombi yangu,
Yasiyotoka katika midomo ya hila.
(K) Nikutazame uso wako katika haki.
Hukumu yangu na itoke kwako,
Macho yako na yatazame mambo ya adili.
Umenijaribu moyo wangu, umenijilia usiku,
Umenihakikisha usione neno;
Nimenuia kinywa changu kisikose.
(K) Nikutazame uso wako katika haki.
Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika,
Utege sikio lako ulisikie neno langu.
Dhihirisha fadhili zako za ajabu,
Wewe uwaokoaye wanaokukimbilia;
Kwa mkono wako wa kuume
Uwaokoe nao wanaowaondokea.
(K) Nikutazame uso wako katika haki.
Unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako;
mimi nikutazame uso wako katika haki,
Niamkapo nishibishwe kwa sura yako.
(K) Nikutazame uso wako katika haki.
Yn 10 : 27
Aleluya, aleluya,
Kondoo wangu waisikia sauti yangu, nami nawajua, nao wanifuata.
Aleluya.
Mt 9:32-39
Walimletea Yesu mtu bubu mwenye pepo. Na pepo alipotolewa, yule bubu alinena, makutano wa kastaajabu, wakasema, Haijaonekana hivi katika Israeli wakati wo wote. Lakini Mafarisayo wakisema, Kwa nguvu za mkuu wa pepo atoa pepo. Naye Yesu alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri habari njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kondoo wasio na mchungaji. Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake.
Maoni
Ingia utoe maoni