Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Sherehe ya Utatu Mtakatifu (Jumapili, Juni 16, 2019)  

Somo la 1

Mit 8 : 22-31

Bwana alikuwa nami katika mwanzo wa njia yake, Kabla ya matendo yake ya kale, Nalitukuka tokea milele, tangu awali, Kabla haijawako dunia. Wakati visipokuwako vilindi nalizaliwa, Wakati zisipokuwako chemchemi zilizojaa maji. Kabla milima haijawekwa imara, Kabla ya vilima nalizaliwa. Alipokuwa hajaiumba dunia, wala makonde, Wala chanzo cha mavumbi ya dunia; Alipozithibitisha mbingu nalikuwako; Alipopiga duara katika uso wa bahari; Alipofanya imara mawingu yaliyo juu; Chemchemi za bahari zilipopata nguvu; Alipoipa bahari mpaka wake, Kwamba maji yake yasiasi amri yake; Alipoiagiza misingi ya nchi; Ndipo nilipokuwa pamoja naye, kama stadi wa kazi; Nikawa furaha yake kila siku; Nikifurahi daima mbele zake; Nikiifurahia dunia inayokaliwa na watu; Na furaha yangu ilikuwa pamoja na wanadamu.

Wimbo wa Katikati

Zab 8:3-8

Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako,
Mwezi na nyota ulizoziratibisha,
Mtu ni kitu gani hata umkumbuke,
Na binadamu hata umwangalie?
(K) Wewe, Mungu, Bwana wetu, Jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!

Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu;
Umemvika taji ya utukufu na heshima;
Umemtawaza juu ya kazi ya mikono yako;
Umevitia vitu vyote chini ya miguu yake.
(K) Wewe, Mungu, Bwana wetu, Jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!

Kondoo, na ng’ombe wote pia;
Naam, na wanyama wa kondeni;
Ndege wa angani, na samaki wa baharini;
Na kila kipitiacho njia za baharini.
(K) Wewe, Mungu, Bwana wetu, Jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!

Somo la 2

Rum 5:1-5

Tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na tuwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ambaye kwa yeye tume- pata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo tunasimama ndani yake; na kufurahi katika tumai- ni la utukufu wa Mungu. Wala si hivyo tu, ila na tufurahi katika dhiki pia; tukijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi; na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini; na tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi.

Shangilio

Ufu 1:8

Aleluya, Aleluya,
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, Mungu ambaye yupo, aliyekuwako, na atakayekuja.
Aleluya.

Injili

Yn 16:12-15

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ningali ninayo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyastahimili hivi sasa. Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. Yeye atanitukuza mimi; kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari. Na yote aliyo nayo Baba ni yangu; kwa hiyo ualisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo yangu, na kuwapasheni habari.

Maoni


Ingia utoe maoni