Jumatano. 27 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumatatu ya 11 ya Mwaka (Jumatatu, Juni 17, 2019)  

Somo la 1

2Kor 6:1-10

Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure. (Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia;tazama,wakati uliokubalika ndiyo sasa; tazama siku ya wokovu ni sasa) Tusiwe kwazo la namna yo yote katika jambo lo lote, ili utumishi wetu usilaumiwe; bali katika kila neno tujipatie sifa njema, kama watumishi wa Mungu; katika saburi nyingi, katika dhiki, katika misiba, katika shida; katika mapigo, katika vifungo, katika fitina, katika taabu, katika kukesha, katika kufunga; katika kuwa safi, katika elimu, katika uvumilivu, katika utu wema, katika Roho Mtakatifu, katika upendo usio unafiki; katika neno la kweli, katika nguvu ya Mungu; kwa silaha za haki za mkono wa kuume na za mkono wa kushoto; kwa utukufu na aibu; kwa kunenwa vibaya na kunenwa vema; kama wadanganyao, bali tu watu wa kweli; kama wasiojulikana, bali wajulikanao sana; kama wanaokufa, kumbe tu hai; kama wanaorudiwa, bali wasiouawa; kama wenye huzuni, bali siku zote tu wenye furaha; kama maskini, bali tukitajirisha wengi; kama wasio na kitu, bali tu wenye vitu vyote.

Wimbo wa Katikati

Zab 98:1-4

Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
(K) Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake

Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli.
(K) Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake

Miisho yote ya dunia imeuona Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi.
(K) Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake

Shangilio

Efe. 1:17,18

Aleluya, aleluya,
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristu, awape roho ya hekima mjue tumaini la mwito wake.
Aleluya.

Injili

Mt 5:38-42

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa jicho, na jino kwa jino; Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili. Na mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia. Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili. Akuombaye, mpe; naye atakaye kukopa kwako, usimpe kisogo.

Maoni


Ingia utoe maoni