Alhamisi, Oktoba 25, 2018
Alhamisi, Oktoba 25, 2018,
Juma la 29 la Mwaka wa Kanisa
Ef 3:14-21
Zab 32:1-2, 4-5, 11-12, 18-19
Lk 12: 49-53
MUNGU NI MOTO UNAOPENDEZESHA VYOTE.
Yesu aliwashtuwa wafuasi wake pale aliposema kuwa amekuja kutupa moto na kusababisha mgawanyiko badala ya amani duniani. Je, ni aina gani ya moto ambao Yesu alikuwanao akilini mwake? Moto katika neno la Kibiblia ulihusianishwa na Mungu pamoja na kuhusianishwa na matendo yake ulimwenguni katika maisha ya watu wake. Wakati mwingine Mungu anadhihirisha uwepo wake kwa uwepo wa moto, kama vile kichaka kiwakacho ambacho hakiteketei alipoongea na Musa (Kut 3:2). Alama ya moto ilitumika pia kuwakilisha utukufu wa Mungu (Eze 1:4, 13), uwepo wa ulinzi wake (2Fal 6:17), utakatifu wake (Kum 4:24), hukumu ya haki (Zek 13:9), na hasira yake dhidi ya dhambi (Isa 66:15-16). Pia imetumika pia ikimaanisha Roho Mtakatifu (Mt 3:11 na Mat 2:3). Moto wa Mungu unasafisha na huondoa uchafu, na unavuvia mwanga na hofu ya kumuabudu Mungu na nguvu ya neno lake ndani yetu.
Basi tuchukue mfano mmoja kutoka kwenye Biblia uhusuo moto – kichaka kiwakacho katika kitabu cha Kutoka. Kichaka chaonekana kuwa kinawaka tu badala ya kuteketea. Sifa ya asili ya moto ni kuchoma na kuteketeza. Lakini kinachotokea hapa ni hali ya tofauti. Je, unasema nini juu ya Mungu wetu? Ndio Mungu wetu ni moto, sio moto uharibuo bali moto unaobadilisha. Unatuunguza sisi kufikia uzuri. Mara utakapo unguzwa na moto huu katika uhalisia unakuwa kiumbe kipya, unatoka kwenye uovu na kusimama njee. Kama upo katika familia yako ya watu wanne na ukawa umeunguzwa mpaka kufikia uzuri katika uhalisia utakuwa nje. Unasimama njee ukiwa tofauti na hapo huenda ukachukiwa au kupendwa au kuigwa. Inawezekana familiya yetu na marafiki zetu kuwa maadui zetu. Kama mawazo yao yatatuzuia sisi kutenda yale tunayoyajua kuwa Mungu anapenda sisi kuyafanya ni dhahiri tutamtii Mungu zaidi kuliko wao, na hapo huenda uadui ukawepo. Je, upendo wa Yesu Kristo unakusukuma wewe kumuweka Mungu kwanza kwa yale yote uyatendayo (2 Kor 5:14)?
Sala:
Bwana, naomba upendo wako unitawale na uyarekebishe maisha yangu.
Amina
Maoni
Ingia utoe maoni