Jumamosi, Septemba 03, 2016
Jumamosi, Septemba 3, 2016,
Juma la 22 la Mwaka wa Kanisa
Kumbukumbu ya Mt. Greogori Mkuu, Papa na Mwalimu wa Kanisa
1Kor 4: 6-15;
Zab144: 17-21;
Lk 6: 1-5
KUFANYA LISILO HALALI SIKU YA SABATO?!
Sabato ilikuwepo hata kabla Torati haijatolewa katika Mlima Sinai (Kut 19). Wayahudi walifundishwa “kukumbuka siku ya Sabato” na kuifanya takatifu. Siku ya sabato ilitegemewa kuwa siku ya mapumziko na siku ya kuabudu, muda wa kukumbuka siku aliyo pumzika Mungu baada ya kazi ya uumbaji, siku ya saba. Mafarisayo walichukulia kitendo walichofanya wafuasi kwenye Injili kuwa ni kufuru kuhusu Sabato. Walivyomlaumu Yesu kuwa ameikufuru Sabato, Yesu aliwajjibu vyema. Yesu alimtumia Daudi kama mfano, wakati Daudi akimkimbia Sauli alikula mikate ile ya Wonyesho (iliobarikiwa) inayotumika tu pale Mahali Patakatifu (tabernacle) ambayo ililiwa na makuhani pekee. (Sam 21: 1-6). Yesu anasema wazi kwamba Sabato sio Bwana, bali Mwana wa mtu (Yesu mwenyewe) ndiye. Ni yeye mwenyewe mwenye mamlaka ya kubadili torati na sheria ya Sabato.
Yesu anatufundisha tusifungwe mno na sheria tushindwe kuonesha upendo kwa jirani zetu. Pamoja na kutimiza majukumu yetu, tusisahau kwamba sisi tunayo sheria ya Kristo ambayo ni upendo, sheria isiyo na upendo si sheria ya Kristo. Mt. Greogori mkuu, alitambua hilo ndio maana alitoa huduma bora katika kanisa, na zaidi sana upendo wake kwa fukara uliomdhihirisha kuwa yeye ni kiongozi na mchungaji wa kweli. Tumuombe atuombee kwa Mungu ili nasi tuweze kuwa na roho ya kuwapenda wote wasiojiweza tuwe na moyo wa kuwahudumia kwa upendo bila kujali jamii inaniona je. Ndugu zangu sisi tunalo deni, na deni letu ni Upendo kwa Mungu na jirani zetu, tujaribu kulilipa kila siku tuwapo hapa duniani.
Sala: Bwana, naomba nikuheshimu katika kazi yangu na katika mapumziko yangu na niwatendee jirani zangu kwa heshima na upendo. Niweke mbali na roho ya mabishano na ubinafsi ili niweze kutafuta uzuri wa jirani zangu katika hali zote. Amina
Maoni
Ingia utoe maoni